Hamas yasisitiza hatima ya pamoja ya muqawama wa Palestina na Hizbullah
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36561-hamas_yasisitiza_hatima_ya_pamoja_ya_muqawama_wa_palestina_na_hizbullah
Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema katika radiamali yake kwa taarifa ya karibuni ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) dhidi ya chama cha Hizbullah kuwa hatima ya muqawama wa Palestina na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imefungamana pamoja.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Nov 20, 2017 10:38 UTC
  • Hamas yasisitiza hatima ya pamoja ya muqawama wa Palestina na Hizbullah

Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema katika radiamali yake kwa taarifa ya karibuni ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) dhidi ya chama cha Hizbullah kuwa hatima ya muqawama wa Palestina na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imefungamana pamoja.

Musa Abu Marzouq amesisitiza kuwa ajenda ya mazungumzo kati ya makundi ya Palestina ni kukabiliana na baadhi ya nchi za Kiarabu kwa hatua yao ya kuitaja harakati ya Hizbullah ya Lebanon kuwa ni kundi la kigaidi. Abu Marzouq amebainisha kuwa misimamo ya kisiasa ya Waarabu inapasa kuelekezwa kwa suala la Palestina na Quds Tukufu. 

Musa Abu Marzouq, Afisa wa ngazi ya juu wa Hamas 

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu jana walitoa taarifa katika kikao chao walichofanya huko Cairo Misri kufuatia ombi la utawala wa Saudia Arabia bila ya kushiriki Qatar, Lebanon, Syria, Iraq, Algeria na Oman na kuitaja harakati ya Hizbullah kuwa ni taasisi ya kigaidi. Harakati hiyo imekuwa na nafasi muhimu katika vita dhidi ya ugaidi wa kitakfiri na Uzayuni. 

Hii ni katika hali ambayo Gebran Bassil Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon amesema kuwa Hizbullah na muqawama ni sehemu muhimu ya taifa la Lebanon. 

Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina pia imetoa taarifa ikilaani taarifa ya Arab League na kueleza kuwa ilitarajiwa kwamba taarifa hiyo ya nchi za Kiarabu ingelaani jinai za utawala ghasibu unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu na uvamizi wa kila uchao wa Israel dhidi ya Wapalestina na ardhi yao, lakini kinyume chake mhimili wa muqawama ndio uliolaaniwa mkabala na utawala wa Kizayuni.