Lebanon na Syria katika mkondo wa kuimarisha uhusiano
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36769-lebanon_na_syria_katika_mkondo_wa_kuimarisha_uhusiano
Saad Zakhia, balozi mpya wa Lebanon nchini Syria alionana na Rais Bashar al Assad siku ya Alkhamisi na kukabidhi hati zake za utambulisho.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 25, 2017 02:38 UTC
  • Lebanon na Syria katika mkondo wa kuimarisha uhusiano

Saad Zakhia, balozi mpya wa Lebanon nchini Syria alionana na Rais Bashar al Assad siku ya Alkhamisi na kukabidhi hati zake za utambulisho.

Lebanon ni nchi ndogo ya Kiarabu lakini ni muhimu katika eneo la Mashariki ya Kati. Moja ya mambo yanayoifanya nchi hiyo kuwa muhimu ni nafasi yake ya jiografia ya kisiasa na nafasi yake katika kambi ya muqawama.

Kwa upande wa jiografia ya kisiasa, Lebanon inapakana na Syria upande wa kaskazini na mashariki; upande wake wa magharibi iko bahari ya Mediterranean huku mipaka yake ya kusini ikiwa imeshikana na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Nafasi hiyo ya kijiografia imeifanya Lebanon muda wote kuwa na muundo wa utulivu na ukosefu wa utulivu kwa wakati mmoja. Hii ni kwa sababu Lebanon haiathiriwi tu na matukio ya Syria na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, bali mara zote inakumbwa na uingiliaji wa Saudi Arabia katika masuala yake ya ndani.

Mpaka wa Lebanon na Syria

 

Tangu ulipozushwa mgogoro wa Syria mwaka 2011, Lebanon nayo iliingia katika mgogoro. Kwa upande mmoja vitendo vya kigaidi na ukosefu wa usalama vilivyokuwa vinatokea Syria vilifika pia ndani ya maeneo tofauti ya Lebanon. Moja ya sababu kubwa zilizoifanya Hizbullah ya Lebanon kutuma wanamapambano wake nchini Syria ni kulinda usalama wa Lebanon, kwani magenge ya kigaidi yaliyokuwa yakifanya jinai ndani ya ardhi ya Syria, yaliendesha vitendo vya kigaidi pia ndani ya ardhi ya Lebanon. Katika upande mwingine, nchi zinazoipinga serikali ya Syria na hasa Saudi Arabia ziliingilia waziwazi masuala ya utawala ndani ya Lebanon na kuishinikiza nchi hiyo ikate uhusiano wake na Syria. 

Mashinikizo hayo yaliharibu uhusiano wa Lebanon na Syria na kupunguza kiwango cha uhusiano wa kidiplomasia kutoka balozi kamili hadi kuwa na balozi mdogo kuanzia mwaka 2013 na kuendelea. Aidha uingiliaji huo wa madola ya kigeni nchini Lebanon ulikwamisha mchakato wa kupatikana rais mpya na nchi hiyo iliendeshwa bila ya rais kwa muda wa miezi 29, kuanzia mwezi Mei 2014 hadi mwezi Oktoba 2016. Kuanzia mwezi Oktoba 2016 wakati alipochaguliwa Michel Aoun kuwa rais mpya na kumalizika mgogoro wa kisiasa nchini Lebanon, na pia kuchaguliwa Saad Hariri kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo, uhusiano wa Beirut na Damascus ulianza pole pole kurejea katika hali yake ya kawaida. 

Rais Bashar al Assad wa Syria katika mazungumzo na balozi mpya wa Lebanon, Saad Zakhia mjini Damascus

 

Mwezi Oktoba 2017, Hussein al Haj Hassan, waziri wa viwanda na Ghazi Zaitar, waziri wa kilimo wa Lebanon waliongoza ujumbe wa makumi ya wafanyabiashara na wanauchumi wa Lebanon kushiriki katika maonyesho ya kimataifa ya mjini Damascus, Syria. Naye Saad Zakhia akateuliwa kuwa balozi mpya wa Lebanon nchini Syria baada ya kupita miaka minne bila ya kuweko balozi kamili wa Lebanon mjini Damascus, na siku ya Alkhamisi, Zakhia akawa rasmi balozi wa Lebanon nchini Syria baada ya kukabidhi hati zake za utambulisho kwa Rais Bashar al Assad wa nchi hiyo.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, moja ya sababu zilizopelekea kuboreka uhusiano wa Lebanon na Syria katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni kutokana na kubainika kwamba kadiri hali ya ukosefu wa usalama inavyoendelea nchini Syria ndivyo Lebanon inavyozidi kupata madhara. Mbali na machafuko ya Syria kuhatarisha usalama wa Lebanon, yamepelekea wimbi kubwa la wakimbizi kuingia ndani ya ardhi ya Lebanon suala ambalo limekuwa ni mzigo mzito kwa nchi ndogo ya Lebanon. Wachambuzi hao wa mambo wanasema pia kuwa, hatua ya Lebanon ya kurejesha balozi wake mjini Damascus ina maana ya kutambua rasmi uhalali wa serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria na kufeli njama za maadui wa nchi hizo mbili za kutaka kuzusha mifarakano na mizozo baina ya mataifa hayo mawili ndugu.