Ufaransa: Bashar al-Assad haendi popote, ataendelea kuongoza
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema hali halisi ya Syria ni kwamba Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo ya Kiarabu ataendelea kubakia madarakani kwa kuwa wapinzani wake wameshindwa 'katika mapambano ya ardhini'.
Katika mahojiano na kanali ya televisheni ya France 24 jana Jumapili, Macron alisema Rais Assad ataendelea kuiongoza nchi hiyo kwa kuwa yupo chini ya himaya ya Iran na Russia.
Amesema serikali ya Paris inataka kuona mwaka mpya wa 2018 ukianza kwa kuandaliwa mazingira ya kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu, kwa kuzishirikisha pande zote.
Hata hivyo amekariri msimamo wa Ufaransa wa huko nyuma, wa kudai kuwa Bashar ni 'adui wa wananchi' ambaye anapaswa kuwajibishwa mbele ya mahakama za kimataifa.
Serikali ya Damascus imekuwa ikikariri kuwa, ushirikiano wa Russia, Iran na Syria umeimarisha mhimili wa muqawama na mapambano dhidi ya njama za Kizayuni na Marekani katika eneo.
Russia imeikosoa mara nyingi Marekani kwa hatua yake ya kuyaunga mkono makundi ya kigaidi huko Syria ili kufanikisha malengo yake nchini humo.