Uturuki yawaonya raia wake dhidi ya kusafiri Marekani, kisa usalama
Uturuki imewapa tahadhari raia wake dhidi ya kusafiri nchini Marekani kutokana na kile inachokitaja kuwa sababu za kiusalama.
Sambamba na kushtadi mzozo kati ya Washington na Ankara, taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imewataka raia wa nchi hiyo kuangalia upya suala la wao kusafiri kwenda Marekani, kutokana na kushtadi mashambulizi ya kigaidi na hujuma za utumiaji mabavu.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mbali na kuongezeka mashambulizi yanayochochewa na chuki za kibaguzi nchini Marekani, lakini pia kumeshuhudiwa ongezeko la kukamatwa kiholela raia wa Uturuki katika nchi hiyo.
Siku ya Jumatano, Marekani iliwataka raia wake wajizuie kusafiri katika nchi za Uturuki, Sudan, Pakistan na Guatemala kwa madai kuwa watahatarisha usalama wao.
Marekani na Uturuki zimekuwa katika msuguano na malumbano kwa muda mrefu sasa. Ankara imekuwa ikiituhumu Washington kwamba ilihusika na mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli tarehe 15 Julai mwaka 2016.
Mbali na Uturuki kuwakamata majasusi wa Marekani wanaotuhumiwa kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi, lakini pia imekuwa ikiishinikiza Washington imrejeshe nyumbani Fethullah Gülen, hasimu mkubwa wa Rais Recep Tayyip Erdoğan nchini Uturuki, anayedaiwa kuratibu mapinduzi hayo yaliyofeli.