Rais Assad: Matatizo ya Waarabu yanasababishwa na fikra potovu
Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema kuwa, matatizo yanayoukumba ulimwengu wa Kiarabu yanatokana na fikra potovu na kwamba madamu tatizo hilo halijatatuliwa, basi bado migogoro na vita vitaendelea kushuhudiwa katika eneo la Mashariki ya Kati.
Rais Assad aliyasema hayo Jana mbele ya viongozi wa ngazi tofauti wakiwemo pia malenga na waandishi wa Kiarabu mjini Damascus ambapo sambamba na kuashiria matatizo ya kiutamaduni na kifikra yaliyoathiri jamii ya Kiarabu alisema, ni lazima kupatikane mabadiliko ya kifikra katika jamii ya Kiarabu.
Rais wa Syria aliongeza kwa kusema kuwa, mabadiliko ya kifikra katika jamii ya Kiarabu yanahitajia mwelekeo mpya kupitia mazungumzo ya kistratijia kati ya wasomi ili kuifahamisha jamii hiyo vipaumbele muhimu. Amezungumzia harakati ya kizazi kipya cha vijana kuelekea makundi yenye misimamo ya kufurutu ada na kufuata Umagharibi na udharura wa kuwekwa wazi ramani ya utamaduni sahihi katika zama hizi na kusema, muqawama asilia ni muqawama wa kifikra na juhudi kupitia kuimarisha utambulisho na kwamba moja ya sababu za muqawama wa wananchi wa Syria ni fikra hiyo.
Amesisitiza kuwa hiyo ni kwa kuwa vita vya Syria vinahesabika kuwa vita vya kifikra na kipropaganda. Mgogoro wa Syria uliibuka mwaka 2011, baada ya makundi ya kigaidi na kitakfiri yanayoungwa mkono na Marekani, Israel na baadhi ya nchi za Magharibi na Kiarabu kuvamia taifa hilo la Kiarabu kwa lengo la kubadili mlingano wa kieneo kwa maslahi ya utawala wa Israel. Hata hivyo njama hizo zimeambulia patupu kutokana na uungaji mkono wa wananchi kwa serikali na pia msaada wa muqawama kwa taifa hilo.