Hizbullah: Tumejiandaa dhidi ya hatua mbaya zozote za Marekani
Mwakilishi wa bunge na mjumbe wa ngazi ya juu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon amesema kuwa, safari ya hivi karibuni ya ujumbe wa Wizara ya Fedha ya Marekani mjini Beirut, ni ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala ya Lebanon na kwamba Hizbullah imeshajiandaa kukabiliana na hatua mbaya zozote za Marekani dhidi yake.
Jumatatu iliyopita Marshall Billingsley, Naibu Waziri wa Fedha wa Marekani akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu alifanya safari mjini Beirut, mji mkuu wa Lebanon na kukutana na viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo akiwemo pia Rais Michel Aoun, Saad Hariri, Waziri Mkuu na Nabih Berri, Spika wa Bunge wa taifa hilo la Kiarabu. Safari ya ujumbe huo wa Marekani nchini Lebanon imefanyika ikiwa ni baada ya kupita karibu wiki mbili tangu Wizara ya Sheria ya Marekani ilipounda kamati ya kuchunguza vyanzo vya fedha vya Harakati ya Hizbullah.
Kamati hiyo iliundwa kupitia madai ya uongo ya Marekani kwamba, harakati hiyo inahusika na mtandao wa biashara ya madawa ya kulevya na utakatishaji fedha. Kufuatia hali hiyo Hussain Al-Musawi, mwakilishi wa bunge na mjumbe wa ngazi ya juu wa harakati hiyo amesisitiza kwamba, Marekani inashindwa kuchukua maamuzi dhidi Hizbullah, kwa sababu ina hatihati; na sababu ya hali ni kutokuwa na uwezo wa kuchukua uamuzi huo au kutokuwa tayari kuyakubali matokeo mabaya ya kuchukua uamuzi huo. Al-Musawi amefafanua kuwa, Hizbullah ni harakati yenye nguvu ambapo imejiandaa kwa machaguo ya kukabiliana na hatua zozote mbaya za Marekani dhidi yake.
Kabla ya hapo pia Sayyid Hassan Nasurullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon alisema kuwa, madai ya Marekani kwamba harakati hiyo inahusika na mtandao wa magendo ya biashara ya madawa ya kulevya au utakatishaji fedha, ni madai yasiyo na msingi kwa kuwa Hizbullah inaamini juu ya uharamu wa mihadarati.