Saudia na Imarati zawafanya mamluki maelfu ya vijana wa Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i43254-saudia_na_imarati_zawafanya_mamluki_maelfu_ya_vijana_wa_afrika
Gazeti la al-Quds al-Arabi limeripoti kuwa, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zinataka kuwasajili maelfu ya vijana wa Kiafrika zitakaowatumia katika operesheni zao za nje ya nchi vikiwemo vita dhidi ya Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 17, 2018 09:33 UTC
  • Saudia na Imarati zawafanya mamluki maelfu ya vijana wa Afrika

Gazeti la al-Quds al-Arabi limeripoti kuwa, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zinataka kuwasajili maelfu ya vijana wa Kiafrika zitakaowatumia katika operesheni zao za nje ya nchi vikiwemo vita dhidi ya Yemen.

Duru za habari zimeliambia gazeti hilo la Kiarabu kuwa, Riyadh na Abu Dhabi zinawasajili vijana wa Kiafrika hususan raia wa Chad, na kuwatumia kama mamluki katika operesheni mbalimbali za nje ya nchi. 

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, mapema mwezi huu Rais Idriss Déby wa Chad alienda Saudia ambapo Riyadh na N’Djamena zilisaini makubaliano ya siri ya kuwasajiliwa vijana wa nchi hiyo ya Kiafrika katika jeshi la Saudi.

Kanali ya televisheni ya al-Masirah ya Yemen imeripoti kuwa, Imarati nayo inataka kuwasajili maelfu ya mamluki raia wa Uganda, itakaowatuma katika nchi za Somalia na Yemen.

Baadhi ya miili ya mamluki wa Sudan waliouawa Yemen

Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Abu Dhabi, Mohammed bin Zayed Al Nahyan anaripotiwa kujiandaa kwenda Uganda karibuni hivi, ambapo miongoni mwa mambo atakayosaini na viongozi wa Kampala ni kuwachukua askari 10,000 wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki na kuwapeleka Imarati, ambapo elfu 8 miongoni mwao watatumwa Yemen na waliosalia watatumwa Somalia.

Si vibaya kuashiria hapa kuwa, Mkuu wa Kikosi cha Sudan kinachoshirikiana na muungano wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen, Mohammed Hamdan Hamidati hivi karibuni aliliambia gazeti la Sudan la al-Jarida kwamba, mamia ya mamluki raia wa Sudan wameuawa kufikia sasa katika uvamizi wa muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya jirani yake Yemen.