Kuendelea madai ya kichekesho ya Netanyahu kuhusu Iran
Waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Jumatatu usiku, katika maonyesho yake mapya ya kipropaganda dhidi ya Iran, ameonyesha picha, CD na karatasi na kudai ni nyaraka zisizopingika kuhusu kile alichodai kuwa eti ni mpango wa siri wa Iran wa kuunda bomu la atomiki.
Pasina kuashiria ukweli kuwa utawala haramu wa Israel unamiliki mamia ya vichwa vya silaha hatari za nyuklia, Netanayhu amedai kuwa eti Iran imeshadidisha mpango wa kuunda bomu la nyuklia.
Maonyesho hayo ya kipropagnada na kichekesho ya Netanyahu yanatolewa katika hali ambayo, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, hadi sasa umethibitisha mara kadhaa kuwa shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa malengo ya amani.
Akijibu matamshi hayo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi jana usiku alisema maonyesho hayo ya kichekeso ya Netanyahu kuhusu Iran ni aina ya kutapatapa kusiko na chochote isipokuwa kueneza uongo na hadaa.
Qassemi amesisitiza kuwa, ili kuendelea kubakisha utawala wao haramu, wakuu wa utawala wa Kizayuni wanatumia hadaa na ujanja kama ule wa zama za Ujahiliya au ujinga na kuongeza kuwa: "Netanyahu na utawala wa Kizayuni unaowaua watoto wanapaswa kufahamu kuwa watu wa dunia wana akili na uwezo wa kutosha wa kubaini mambo."
Naye Sayyed Abbas Araqchi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema nyaraka ambazo Netanyahu amezionyesha ni bandia na za kujibunia. Amesema kitendo hicho cha Netanyahu kinalenga kuathiri maamuzi ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Netanyahu ametoa madai hayo katika hali ambayo, madai yaliyokuwa yametolewa huko nyuma na Marekani kuhusu shughuli za nyuklia za Iran za miaka iliyopita maarufu kama faili la PMD yalifungwa wakati mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji yalipofikiwa Julai mwaka 2015 baina ya Iran na wanachama tano wa kudumu wa Baraza la Usalama pamoja na Ujerumani.
Kwa upande wake Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini, usiku wa kuamkia leo amejibu mchezo wa kitoto wa Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel aliyedai kuwa eti Iran haijaheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Amesema IAEA imeshathibitisha mara 10 hadi sasa kuwa Iran inafungamana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Madai ya Netanyahu yametolewa baada ya safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo mjini Tel Aviv na ni ishara kuwa Trump anapanga kuondoa nchi yake katika mapatano ya JCPOA.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Jawad Zarif naye ametuma ujumbe katika akaunti yake ya Twitter na kusema madai yasiyo na msingi ya Trump yanakuja wakati wa kukaribia maamuzi ya Trump kuhusu JCPOA mnamo Mei 12. Zarif amemtaja Netanayhu kuwa mtoto anayelia bila sababu na kuongeza kuwa mtawala huyo wa Israeli hawezi kuwahadaa watu wakati wote.
Ikumbukwe kuwa miaka 6 iliyopita katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Netanyahu alionyesha ramani na kudai kuwa eti Iran inakaribia mstari mwekundi wa kumiliki bomu la nyuklia. Madai hayo yalipuuzwa na jamii ya kimataifa.