Saudia yawakamata wanaharakati waliopigania haki ya wanawake kuendesha gari nchini humo
(last modified Fri, 18 May 2018 14:46:00 GMT )
May 18, 2018 14:46 UTC
  • Saudia yawakamata wanaharakati waliopigania haki ya wanawake kuendesha gari nchini humo

Utawala wa Aal-Saud umewatia mbaroni wanaharakati kadhaa wengi wao wakiwa wa kike, walioongoza kampeni za kutaka kuruhusiwa wanawake kuendesha magari nchini Saudi Arabia.

Shirika la habari la Reuters limenukuu mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Saudia yakisema kuwa, "Wimbi hili jipya la kamatakamata linalenga kuwazuilia wanaharakati waliopigania haki ya wanawake kuendesha gari, ili wasiendelee kujisifu kuwa ruhusa hiyo imetolewa huko Saudia kutokana na jitihada zao."

Kwa akali wanaharakati watano wamekamatwa kufikia sasa. Wanawake nchini Saudi Arabia wataanza kuruhusiwa kuendesha magari tarehe 24 mwezi ujao wa Juni. 

Septemba mwaka jana, na baada ya malalamiko ya muda mrefu, hatimaye Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal-Saud wa Saudi Arabia alitoa amri ya kuwapa leseni za kuendesha magari wanawake wa nchi hiyo.

Wanawake wa Saudia baada ya kuruhusiwa kuendesha gari

Tangu mwaka 1957, wanawake wa Saudia wamenyimwa uhuru wa kuendesha gari ndani ya nchi hiyo, kufuatia amri kali iliyopiga marufuku suala hilo, na ambao wamekuwa wakikuka sheria hiyo wamekiwa wakikabiliwa na adhabu kali ikiwemo kuchapwa viboko.

Katika kukaribia kumkabidhi madaraka mwanawe, Mohammad Bin Salman hivi sasa Mfalme Salman bin Abdulaziz anakusudia kufuta baadhi ya sheria ambazo zimekuwa zikikosolewa ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kumsafishia njia mwanawe huyo asiweze kukabiliana na changamoto zaidi pindi atakapochukua uongozi.

Tags