Amnesty na HRW zaitaka Saudia iwaachie huru wanaharakati 7 wanawake
(last modified Sun, 20 May 2018 07:17:10 GMT )
May 20, 2018 07:17 UTC
  • Amnesty na HRW zaitaka Saudia iwaachie huru wanaharakati 7 wanawake

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yameutaka utawala wa Aal-Saud uwaachie huru wanaharakati saba wa kike walioongoza kampeni za kutaka kuruhusiwa wanawake kuendesha magari nchini Saudi Arabia.

Sarah Leah Whitson, Mkurugenzi wa Human Rights Watch eneo la Mashariki ya Kati sanjari na kuitaka Riyadh iwaachie huru wanaharakati hao, amesema, "Inavyoonekana, kosa walilofanya wanawake hao ni kutaka wanawake waruhusiwe kuendesha magari, kabla hajataka Mohammed bin Salman (Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia).

Naye Samah Hadid, Mkurugenzi wa Kampeni eneo la Mashariki ya Kati wa Amnesty International amesema Saudia haipaswi kuendelea kudai kuwa inapigania haki za wanawake na mageuzi, ilhali inawalenga watetezi wa haki hizo ambao wanatekeleza uhuru wao wa kujieleza, kutangamana na kujumuika.

Shirika la habari la Reuters limenukuu mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Saudia yakisema kuwa, "Wimbi hilo jipya la kamatakamata linalenga kuwazuilia wanaharakati waliopigania haki ya wanawake kuendesha gari, ili wasiendelee kujisifu katika vyombo vya habari kwamba ruhusa hiyo ilitolewa huko Saudia kutokana na jitihada na harakati zao."

Mmoja wa wanaharakati wa kike waliopigania haki ya wanawake kuruhusiwa kuendesha magari Saudia

Septemba mwaka jana, na baada ya harakati na malalamiko ya muda mrefu, hatimaye Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal-Saud wa Saudi Arabia alitoa amri ya kuwapa leseni za kuendesha magari wanawake wa nchi hiyo.

Hata hivyo ruhusa hiyo ya wanawake kuendesha magari nchini Saudi Arabia itaanza kutekelezwa tarehe 24 mwezi ujao wa Juni. 

Tags