Jul 17, 2018 16:38 UTC
  • Ripoti: Askari vamizi wa Imarati wanawateka na kuwabaka wanawake wa Yemen

Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kwamba, vitendo vya kutekwa nyara wasichana wa Yemen na kubakwa katika maeneo yanayodhibitiwa na askari vibaraka na vamizi wanaoungwa mkono na kufadhiliwa na serikali ya Imarati, vimeongezeka zaidi.

Baadhi ya ripoti zinaeleza kwamba, wiki iliyopita wasichana wawili walio na umri wa chini ya miaka 20, walitekwa nyara na askari wanaoungwa mkono na serikali ya Abu Dhabi na kuwabaka. Wazazi wa wasichana hao pia walitishiwa usalama wao kwamba, iwapo watafichua watu waliowateka nyara watoto wao, watauawa. Kwa mujibu wa taarifa zilizoufikia mtandao wa habari wa Murasil Net, askari wa Imarati wanasimamia kundi la maafisa kadhaa wa usalama vibaraka ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kuwateka nyara mabinti wa Yemen na kisha kuwakabidhi kwa askari hao vamizi.

Askari vamizi wa Imarati wanaofanya ubakaji na jinai dhidi ya raia madhlumu wa Yemen

Amani Ibrahim Omar, raia wa Yemen amenukuliwa akisema kuwa, wiki iliyopita binti yake alitekwa nyara na maafisa wa polisi walio chini ya usimamizi wa askari wa Imarati na kudhalilishwa kijinsia. Aidha mwanzoni mwa mwezi huu wa Julai wasichana wengine kadhaa wa eneo la al-Mansurah la mji wa Aden, huko kusini mwa Yemen walitekwa nyara na kudhalilishwa kijinsia. Baadhi ya duru za habari nchini Yemen zimetangaza kwamba, watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii kunaofichua na kulaani jinai za askari wa Imarati za kuwateka nyara na kuwabaka wasichana wa nchi hiyo ya Kiarabu, wanakamatwa na kusweka katika katika jela za siri za  Imarati. Ripoti zinaeleza kwamba askari wa Imarati wanamiliki jela 18 za siri huko kusini mwa Yemen ambapo karibu Wayemen 2000 wanashikiliwa. Maeneo ya Yemen kusini yanashibitiwa na askari wa muungano vamizi wa Saudia pamoja na makundi ya kigaidi kama vile al-Qaidah na askari wa Imarati.

Tags