Mtawala wa Dubai awashambulia viongozi wa nchi za Kiarabu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47247-mtawala_wa_dubai_awashambulia_viongozi_wa_nchi_za_kiarabu
Waziri Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) amesema kuwa wanasiasa wa ulimwengu wa Kiarabu wamefeli katika kuziongoza nchi zao na kusisitiza kuwa, mgogoro uliopo hivi sasa katika nchi za Kiarabu unatokana na uongozi mbaya.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Aug 05, 2018 10:57 UTC
  • Mtawala wa Dubai awashambulia viongozi wa nchi za Kiarabu

Waziri Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) amesema kuwa wanasiasa wa ulimwengu wa Kiarabu wamefeli katika kuziongoza nchi zao na kusisitiza kuwa, mgogoro uliopo hivi sasa katika nchi za Kiarabu unatokana na uongozi mbaya.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Sheikh Muhammad bin Rashid Aal Maktoum akisema hayo katika mtandao wa Twitter na kuongeza kuwa: "Sisi katika ulimwengu wa Kiarabu tuna wanasiasa wengi kama ambavyo hivi sasa mgogoro wa nchi za Kiarabu hautokani na maliasili, bali uongozi mbaya."

Amesema, kitendo cha wanasiasa cha kuzama kupindukia katika siasa kumezitumbukiza nchi za Kiarabu katika ufisadi wa kimaadili na kuangamiza maliasili zake.

Maandamano ya wananchi wa Tunisia kulalamikia uongozi mbaya

 

Matamshi hayo ya mtawala wa Dubai ambaye pia ni waziri mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu yametolewa katika hali ambayo wataalamu wa kisiasa wa eneo hili wanasema kuwa, mgogoro mkubwa wa nchi za Kiarabu ni kutoshirikishwa wananchi katika maamuzi ya nchi zao, kuendeshwa nchi kiukoo, na kushadidi ukandamizaji na hatua kali za kiusalama kwa kila anayethubutu kunyanyua mdomo wake kulaumu utendaji wa tawala za nchi hizo.

Wataalamu hao wameongeza kuwa, hakuwezi kushuhudiwa mabadiliko yoyote ya kimsingi katika nchi za Kiarabu madhali wananchi wataendelea kunyimwa haki zao za kimsingi za kujiamulia wenyewe masuala ya nchi zao.