Wayemen wa mji wa Aden waandamana kulaani hatua haribifu za Imarati
Familia za watu wanaoshikiliwa katika jela za siri za askari wa Imarati nchini Yemen, zimefanya maandamano ya kulaani hatua haribifu za askari hao mjini Aden, kusini mwa Yemen.
Maandamano hayo yamefanyika mbele ya makazi ya Ahmed Al-Misri, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Rais Abdrabbuh Mansur Hadi, Rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu uongozi na kutoroka nchi. Katika maandamano hayo, familia hizo zimekosoa matamshi ya Ali Nasser, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikali hiyo aliyedai kwamba, hakuna jela za siri wala utesaji unaofanywa ndani ya jela za Yemen.
Washiriki wa maandamano hayo pia wameibebesha serikali hiyo ya Abdrabbuh Mansur Hadi dhima ya kukamatwa watoto wao na wametaka kuwekwa wazi mustakabli wa ndugu zao hao. Miji ya kusini ya Yemen imekuwa ikikumbwa na machafuko na ghasia tangu askari wa serikali ya Sana'a kwa kushirikiana na Harakati ya Wananchi ya Answarullah walipoondoka maeneo hayo.