Makumi ya Walowezi wa Kizayuni wavamia Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa
(last modified Fri, 08 Feb 2019 14:52:58 GMT )
Feb 08, 2019 14:52 UTC
  • Makumi ya Walowezi wa Kizayuni wavamia Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa

Makumi ya walowezi wa Kizayuni leo wameuvamia tena Msikiti wa al-Aqswa huko Palestina wakisaidiwa na askari wa jeshi la utawala haramu wa Israel na kuuvunjia heshima msikiti huo mtakatifu na kibla cha kwanza cha Waislamu.

Mtandao wa Habari wa Al'A'had wa Lebanon unaripoti kwamba, walowezi hao baada ya kuingia katika msikiti huo walisikika wakipiga nara dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Hii ni mara ya pili kwa walowezi wa Kizayuni kufanya hujuma dhidi ya msikiti wa al-Aqswa katika kipindi cha ndani ya wiki moja.  Siku ya Jumatano walowezi hao wa Kizayuni waliingia katika msikiti huo mtakatifu kupitia Babul Maghariba na kufanya vitendo vya kichochezi na vya kuuvunjia heshima msikiti huo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, karibu kila siku walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakifanya uvamizi katika msikiti huo lengo likiwa ni kutekeleza njama za kutokomeza utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa Msikiti wa al-Aqswa na badala yake kuweka nembo za Kizayuni.

Askari wa utawala wa kizayuni wa Israel wakivamia msikiti wa al-Aqswa

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya njama za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.

Hata hivyo kusimama kidete wananchi wa Palestina hadi sasa kumekwamisha njama na mipango yote ya Wazayuni, zikiwemo njama zake za kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa Baytul Muqaddas. 

Oktoba mwaka 2017, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO lilitangaza kuwa, Msikiti wa al-Aqswa ni mali ya Waislamu na hauna uhusiano wowote na Mayahudi.