Msimamo wa Oman wa kuiunga mkono Israel wakosolewa na Jordan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i52695-msimamo_wa_oman_wa_kuiunga_mkono_israel_wakosolewa_na_jordan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan ametoa jibu kwa matamshi ya waziri mwenzake wa Oman ya kuuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kwamba, tatizo kuu ni ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na Israel.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Apr 07, 2019 11:25 UTC
  • Msimamo wa Oman wa kuiunga mkono Israel wakosolewa na Jordan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan ametoa jibu kwa matamshi ya waziri mwenzake wa Oman ya kuuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kwamba, tatizo kuu ni ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na Israel.

Akihutubia hapo jana kikao cha kitaalamu cha Jukwaa la Uchumi Duniani kinachofanyika nchini Jordan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Yousuf bin Alawi alitoa matamshi ya kustaajabisha na ambayo hayakutarajiwa, alipowataka Wapalestina watoe dhamana na kuuhakikishia utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa hautakabiliwa na hatari yoyote katika Mashariki ya Kati.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Yousuf bin Aalawi (kushoto) akiamkiana kwa bashasha na Netanyahu

Ayman al-Safadi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan amefafanua katika majibu yake kwa matamshi yaliyotolewa na Bin Alawi kwa kusema: Suala la msingi si kudhamini usalama wa Israel, bali ni ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na utawala huu ghasibu na kuendeleza kwake dhulma na jinai dhidi ya Wapalestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, Ayman al-Safadi

Al Safadi ameongeza kuwa, ikiwa Israel inataka idhaminiwe na kuhakikishiwa usalama wake, lazima iondoke katika ardhi za Waarabu ilizozivamia na kuanza kuzikalia kwa mabavu mwaka 1967 na kuruhusu kuundwa nchi ya Palestina.

Ikumbukwe kuwa mwaka uliopita wa 2018, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu, alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa utawala huo haramu kuitembelea Oman katika kipindi cha miaka 20 iliyopita kwa mwaliko wa mfalme wa nchi hiyo Sultan Qaboos bin Said; na waziri wa mambo ya nje wa Oman Yousuf bin Alawi akatamka kwamba, Israel inakubalika kuwa ni nchi katika Mashariki ya Kati. 

Sultan Qaboos bin Said wa Oman (kulia) alipomkaribisha Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Muscat

Baadhi ya nchi za Kiarabu zimeshughulishwa na suala la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, wakati takwimu zinaonyesha kuwa, tangu mwaka 1967 hadi 2017 utawala huo haramu umewaua shahidi Wapalestina zaidi ya 42,000 mbali na kuwajeruhi na kuwaacha bila makazi mamia ya maelfu ya wengine.../