Uungaji mkono kamili wa Trump kwa jinai za Wazayuni huko Ghaza
Tokea Rais Donald Trump wa Madarakani aingie madarakani 20 January 2017, amekuwa akiuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel bila masharti yoyote na amechukua hatua ambazo marais waliomtangulia wa Marekani hawajawahi kuzichukua katika kuupa himaya utawala huo bandia.
Trump ambaye amepata umaarufu kutokana na utayarifu wake wa kuutumikia utawala wa Kizayuni, mnamo 6 Mei katika hatua ya wazi ya kupendelea upande mmoja, alitangaza kuwa anaunga mkono kikamilifu hatua za utawala wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.
Trump ambaye kwa uungaji mkono wake huo wa wazi ni mshirika wa jinai za utawala wa Kizayuni, katika sehemu moja ya ujumbe wake wa Twitter amewahutubu watu wanaodhulumiwa Palestina kwa kusema: "Kuvurumisha maroketi dhidi ya Israel hakutawaletea chochote isipokuwa masaibu. Sitisheni uhasama wenu na muelekee katika amani. Hili linawezekana."
Trump ameyasema hayo pasina kuzingatia uvamizi wa kikatili ambao utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiutekeleza kwa kila kisingizio dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza ambao wamekuwa chini ya mzingiro kamili wa utawala huo dhalimu kwa miaka mingi sasa. Trump amedai kuwa Wapalestina wa Ghaza wanapaswa kulaumiwa kutokana na hali inayowakabili katika hali ambayo utawala wa Kizayuni umekuwa ukiwahujumu na kuwaua kiholela.
Katika mapigano ambayo yalijiri siku chache zilizopita baina ya makundi ya wapigania ukombozi wa Palestina na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel, hadi sasa Wapalestina wasiopungua 145 wameuawa shahidi na wengine 154 kujeruhiwa. Kufuatia kipigo walichopata Wazayuni baada ya makundi hayo ya Jihadi ya Wapalestina kuwavurumishia makombora Wazayuni na kuwaingiza wahka na kiwewe, utawala wa Kizayuni umelazimika kuomba muafaka wa kusitishwa mapigano.
Katika kipindi cha miaka mitatu sasa, Trump amekuwa akiutumikia utawala wa Kizayuni wa Israel katika kiwango ambacho wakuu wa utawala wa Kizayuni hasa waziri mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu hawakuwa wakitasawari hata katika ndoto zao.
Utawala wa Trump ni muungaji mkono mkuu wa Israel kupitia kuukabidhi utawala huo misaada mbali mbali ya kifedha na silaha na kila mwaka Washington imekuwa ikiupa utawala huo msaada wa dola bilioni 3.8 za kifehda.
Katika upande mwingine, Rais Trump wa Marekani mnamo Machi 25 2019, yaani wiki mbili tu kabla ya uchaguzi wa bunge katika utawala wa Kizayuni, alichukua hatua inayokiuka sheria zote za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kutangaza kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel kama mmiliki wa Miinuko ya Golan ya Syria ambayo utawala huo unaikalia kwa mabavu. Hatua hiyo ilikuwa na nafasi ya kumuwezesha Netanyahu apate ushindi kwa mara nyingine katika uchaguzi.
Mwaka uliopita pia, mnamo Mei 2018, Trump alichukua hatua ya kichochezi na kikiuka maazimio yote ya kimataifa kwa kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Quds Tukufu (Jerusalem), mji ambao unakaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel. Ungaji mkono mwingine wa Trump kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni kukata msaada wa Marekani kwa Wakala wa Umoja wa Mataifa wa Kuwahudumia Wakimbizi Wapalestina (UNRWA), kumtimua balozi wa Palestina mjini Washington na kufunga akaunti za benki za ubalozi huo.

Serikali ya Trump imechukua hatua mpya katika kuunga mkono utawala wa Israel kwa kuzilazimisha nchi ziingine ziache kuupinga utawala huo ghasibu.
Elan Carr, mjumbe maalumu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani katika masuala ya kukabiliana na kile kinachotajwa kuwa ni 'chuki dhidi ya Mayahudi', amenukuliwa akisema: "Marekani itaangalia upya uhusiano wake na nchi ambazo zina misimamo dhidi ya Israel. Tuna wasiwasi mkubwa na nchi ambazo tuna uhusiano nazo na wakati huo huo zina misimamo dhidi ya Israel. Kwa mtazamo wa Marekani chuki dhidi ya Uzayuni na Uyahudi ni kitu kimoja na tumeweka wazi hilo."
Kwa msingi huo, utawala wa Trump umechukua hatua nyingine katika kuuhudumia utawala wa Kizayuni wa Israel. Trump anatumai kuwa kwa kuchukua msimamo kama huo atapata uungaji mkono wa makundi yenye ushawishi mkubwa ya Kizayuni kama vile AIPAC, na hivyo kuvutia kura za Mayahudi katika uchaguzi wa rais wa Marekani wa 2020. Lobi au makundi yenye ushawishi mkubwa ya Kizayuni hasa AIPAC yana nafasi kubwa katika uga wa siasa za Marekani na Trump ana uhusiano mzuri na makundi hayo.