Kufungwa UNRWA; takwa jipya la Marekani dhidi ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i53679-kufungwa_unrwa_takwa_jipya_la_marekani_dhidi_ya_palestina
Rais Donald Trump wa Marekani alipoingia katika ikulu ya nchi hiyo White House, alichukua msimamo wa kuiunga mkono Israel bila ya masharti yoyote na wakati huo huo kudhihirisha uhasama wa waziwazi dhidi ya Wapalestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 24, 2019 00:11 UTC
  • Kufungwa UNRWA; takwa jipya la Marekani dhidi ya Palestina

Rais Donald Trump wa Marekani alipoingia katika ikulu ya nchi hiyo White House, alichukua msimamo wa kuiunga mkono Israel bila ya masharti yoyote na wakati huo huo kudhihirisha uhasama wa waziwazi dhidi ya Wapalestina.

Serikali ya Trump siku baada ya siku imekuwa ikichukua hatua mpya za kuwazidishia mashinikizo wananchi wa Palestina. 

Katika uwanja huo, Jason Greenblatt Mjumbe Maalumu wa Marekani anayeshughulikia masuala ya magharibi mwa Asia siku ya Jumatano ya tarehe 22 mwezi huu alitaka kufungwa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi wa Kipalestina linalosimamiwa na Umoja wa Mataifa UNRWA. Greenblatt amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu eneo la Asia Magharibi kuwa: Umefika wakati sasa wa  kukabidhiwa kwa taasisi zisizo za kiserikali na nchi zinazowapokea wakimbizi wa Palestina huduma zote zinazotolewa na UNRWA. 

Jason Greenblatt, Mjumbe Maalumu wa Marekani anayeshughulikia masuala ya magharibi mwa Asia
 

Amedai kuwa muundo wa shirika la UNRWA  umewapuuza wananchi wa Palestina. Tarehe 31 Agosti mwaka jana serikali ya Trump ilisitisha misaada yake yote ya kifedha kwa UNRWA na kudai kuwa shirika hilo lilikuwa na kasoro. Unrwa iliasisiwa Disemba mwaka 1949 kwa mujibu wa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kwa lengo la kutoa misaada na ajira kwa wakimbizi wa Palestina. Hivi sasa shirika hilo linawahudumia karibu wakimbizi milioni tano wa Kipalestina huko Jordan, Syria, Lebanon na katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na vile vile huko Ukanda wa Ghaza. 

Sami Abu Zuhri Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas aliwahi kusema kuwa: Uamuzi wa Marekani wa kukata misaada ya kifedha kwa shirika la UNRWA umechukuliwa lengo likiwa ni kufutilia mbali haki ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi zao za asili.  

Sami Abu Zuhri, Msemahi wa Harakati ya Hamas

Inaonekana kuwa hatua ya Washington ya kukata misaada yake ya kifedha kwa UNRWA ni sehemu ya siasa za Trump za kuwaongezea mashinikizo Wapalestina ili waukubali mpango unaotajwa kuwa "Muamala wa Karne." Muamala wa Karne ni mpango mpya uliopendekezwa na serikali ya Marekani kwa lengo la kufutilia mbali haki za raia wa Plaestina. Kwa mujibu wa mpango huo, Wapalestina wanapasa kutupilia mbali haki yao ya kurejea katika ardhi zao za jadi; haki ambayo imetambuliwa ndani ya azimio nambari 194 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Mpango huo wa Muamala wa Karne ni kinyume na maazimio ya Umoja wa Mataifa na vile vile sheria za kimataifa. Hata Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambayo hadi sasa imetekeleza hatua nyingi za mapatano na utawala wa Kizayuni, pia inaamini kuwa mpango huo haukubaliki.  

Miezi kadhaa iliyopita Mahmoud Abbas, mkuu wa mamlaka hiyo alisema huko Ramallah katika hotuba aliyoitoa kwa mnasaba wa kuadhimishwa mwaka wa 54 tangu kuasisiwa Harakati ya Fat-h kwamba: Kamwe Hatutamruhusu Rais Donald Trump wa Marekani aiuze Quds kwa Israel.    

Trump ametoa huduma kubwa kwa Israel katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita; huduma ambayo viongozi wa ngazi ya juu wa utawala huo khususan Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu hawakuwahi kuifikiria hata kwenye ndoto zao. 

Serikali hiyo ya Trump inatambulika kama muungaji mkono mkuu wa Israel kupitia misaada mbalimbali ya kifedha na  silaha; ambapo kwa mwaka serikali ya Marekani huipatia Israel msaada wa dola bilioni tatu na milioni 800. Katika upande mwingine, Rais wa Marekani Machi 25 mwaka huu alikubali na kutambua rasmi hatua ya utawala ghasibu wa Israel ya kukalia kwa mabavu miinuko ya Golan ya Syria.   

Miinuko ya Golan nchini Syria
 

Mwaka mmoja kabla ya hapo pia, yaani mwezi Mei mwaka jana serikali ya Trump ilichukua hatua ya kichokozi na inayokinzana na maazimio yote ya Umoja wa Mataifa pale alipotangaza kuuhamishia huko Quds kutoka Tel Aviv ubalozi wa nchi hiyo. Uungaji mkono mwingine wa moja kwa moja wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni unaonekana wazi kupitia hatua yake ya kulikatia misaada shirika la UNRWA, kufukuzwa balozi wa Palestina mjini Washington na kufungwa akaunti ya balozi huyo. Trump sasa ameazimia kukamilisha huduma yake kwa utawala wa Kizayuni kwa kutangaza mpango huo wa Muamala wa Karne na kuutekeleza kivitendo. Kwa msingi huo, takwa la Washington la kufungwa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA) pia linapaswa kuhesabiwa kuwa sawa na kutangazwa rasmi mwanzo wa utekelezwaji wa mpango huo.