Mamluki wa Imarati washambulia msikiti Yemen na kuua watu kadhaa
Mamluki wa Umoja wa Falme za Kiarabu ambao ni sehemu ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia wamevamia msikiti mmoja katika mkoa wa Dhale kusini mwa Yemen na kuua watu sita waliokuwa kwenye nyumba hiyo ya ibada, mbali na kuwateka nyara wengine wanne.
Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya al-Masirah ya Yemen, lengo la hujuma hiyo ya jana Ijumaa ya wapiganaji vibaraka wa Imarati dhidi ya waumini wa Kiislamu waliokuwa wakitekeleza ibada msikitini hapo, halijabainika.
Hata hivyo wadadisi wa mambo wanasema, sababu kuu ya shambulizi hilo dhidi ya msikiti ni kulipizaji kisasi kwa kuzingatia kuwa, makumi ya askari wa muungano huo vamizi wameuawa katika siku za hivi karibuni na jeshi la Yemen kwa kushirikiana na kamati za wananchi.
Vyombo vya habari vya Saudi Arabia vilikiri hapo jana kwamba askari 70 wa nchi hiyo wameuawa katika wiki za hivi karibuni kwenye mpaka wa nchi hiyo na Yemen.
Saudia imekiri hayo siku mbili baada ya Brigedia Jenerali Yahya Sarii ambaye ni msemaji wa Jeshi la Yemen kusema Jumatano iliyopita kwamba, zaidi ya wanajeshi na mamluki 200 wa Saudi Arabia waliangamizwa na wengine kujeruhiwa katika operesheni iliyofanywa na Jeshi la Yemen na wapiganaji wa harakati ya Ansarullah huko Najran.
Maelfu ya raia wa Yemen wameuwa, mamilioni wamelazimishwa kuwa wakimbizi na maelfu ya wengine wamejeruhiwa tangu Saudi Arabia, Imarati na waitifaki wao waanzishe mashambulizi dhidi ya taifa la Yemen mwezi Machi mwaka 2015.