Wayemen waushambulia tena uwanja wa ndege wa kimataifa wa Saudia; mara hii watumia droni tano
(last modified Fri, 14 Jun 2019 07:28:41 GMT )
Jun 14, 2019 07:28 UTC
  • Wayemen waushambulia tena uwanja wa ndege wa kimataifa wa Saudia; mara hii watumia droni tano

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abha wa kusini mwa Saudi Arabia umeshambuliwa tena na jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen.

Televisheni ya al Masirah ya Yemen imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, mapema leo Ijumaa asubuhi, ndege tano zisizo na rubani (droni) aina ya 2K za Yemen zimepenya ndani ya ardhi ya Saudi Arabia na kufanya mashambulizi dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abha.

Kwa mujibu wa televisheni hiyo, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abha huko kusini mwa Saudi Arabia ulilazimika kufungwa baada ya kushambuliwa kwa kombora la cruise la Jeshi na Kamati za Kujitolea za Wananchi wa Yemen juzi Jumatano. 

Jeshi na Kamati za Kujitolea za Wananchi wa Yemen zinasema kuwa zinafanya mashambulizi hayo dhidi ya maeneo muhimu na ya kiistratijia ya Saudi Arabia kujibu jinai za wavamizi hao ambao wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kiholela dhidi ya wananchi wa Yemen na kupelekea kufungwa viwanja vya ndege vya nchi hiyo maskini ya Kiarabu.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abha kusini mwa Saudi Arabia

 

Kabla ya hapo pia Wayemen walikuwa wamezionya Saudia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kwamba zitalazimika kufunga viwanja vyao vya ndege kama zilivyoilazimisha Yemen kufunga viwanja vyake vya ndege kutokana na mashambulizi yao ya kiholela nchini humo.

Itakumbukwa kuwa tangu mwezi Machi 2015, Saudi Arabia na Imarati zinaongoza muungano vamizi unaofanya jinai kubwa dhidi ya wananchi Waislamu wa Yemen kwa zaidi ya miaka minne sasa, hivyo Wayemen wanasema ni haki yao kujibu jinai za wavamizi hao kwa kufanya mashambulizi ndani ya ardhi za Saudia na Imarati.

Tags