MOSSAD: Israel kufungua 'ubalozi wake' nchini Oman
Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel (MOSSAD) amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unatazamiwa hivi karibuni kufungua Ofisi ya Uwakilishi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala huo katili nchini Oman.
Yossi Cohen aliyasema hayo jana Jumatatu katika Kongamano la Herzliya kaskazini mwa mji wa Tel Aviv na kuongeza kuwa, "Hivi karibuni, tuliafikiana na Oman kuhuisha uhusiano wa pande mbili na pia suala la kufungua ofisi ya uwakilishi katika nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi."
Amesema hatua hii ni moja ya ishara za wazi zinazoashiria jitihada chungu nzima zinazofanyika chini kwa chini za kuufanya kuwa wa kawaida uhusiano wa utawala huo katili na nchi za Kiarabu.
Ikumbukwe kuwa, Oktoba mwaka uliopita wa 2018, Benjamin Netanyahu, alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa utawala huo haramu kuitembelea Oman katika kipindi cha miaka 20 iliyopita kwa mwaliko wa mfalme wa nchi hiyo Sultan Qaboos bin Said.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Yousuf bin Alawi amewahi kutamka wazi wazi kwamba, Israel inakubalika kuwa ni nchi katika Mashariki ya Kati.
Oman na Israel ambazo hazina uhusiano wa kidiplomasia, katika miaka ya 1990 zilikubaliana kufungua ofisi za uwakilishi wa kibiashara, lakini mwaka 2000, serikali ya Muscat ikatangaza kuzifunga baada ya kuanza Intifadha ya Pili ya Palestina.
Baadhi ya nchi za Kiarabu zimeshughulishwa na suala la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, wakati takwimu zinaonyesha kuwa, tangu mwaka 1967 hadi 2017 utawala huo haramu umewaua shahidi Wapalestina zaidi ya 42,000 mbali na kuwajeruhi na kuwaacha bila makazi mamia ya maelfu ya wengine.