Oman yakanusha madai ya kutaka kuhuisha uhusiano wake na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54518-oman_yakanusha_madai_ya_kutaka_kuhuisha_uhusiano_wake_na_israel
Serikali ya Oman imekanusha vikali madai ya Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel (MOSSAD) aliyedai kuwa Oman ipo mbioni kuhuisha uhusiano wake wa kidiplomasia na utawala huo haramu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 03, 2019 02:50 UTC
  • Oman yakanusha madai ya kutaka kuhuisha uhusiano wake na Israel

Serikali ya Oman imekanusha vikali madai ya Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel (MOSSAD) aliyedai kuwa Oman ipo mbioni kuhuisha uhusiano wake wa kidiplomasia na utawala huo haramu.

Katika ujumbe uliotumwa kwenye ukurasa rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter na Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman, serikali ya Muscut imeyataja madai hayo kama upotoshaji na yasiyo na msingi.

Taarifa hiyo imesema kuwa, "Utawala wa Kisultani wa Oman unaunga mkono jitihada zote za kieneo na kimataifa za kupatikana amani baina ya Palestina na Israel, lakini jitihada tu ambazo zitapelekea kuundwa dola huru la Palestina."

Jumatatu iliyopita, Yossi Cohen Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel (MOSSAD) alisema utawala wa Kizayuni wa Israel unatazamiwa hivi karibuni kufungua Ofisi ya Uwakilishi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala huo katili nchini Oman.

Alidai kuwa: "Hivi karibuni, tuliafikiana na Oman kuhuisha uhusiano wa pande mbili na pia suala la kufungua ofisi ya uwakilishi katika nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi. Hatua hii ni moja ya ishara za wazi zinazoashiria jitihada chungu nzima zinazofanyika chini kwa chini za kuufanya kuwa wa kawaida uhusiano wa utawala huo katili na nchi za Kiarabu."

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel alipokutana na Sultan Qaboos bin Said wa Oman mjini Muscat

Ikumbukwe kuwa, Oktoba mwaka uliopita wa 2018, Benjamin Netanyahu, alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa utawala huo haramu kuitembelea Oman katika kipindi cha miaka 20 iliyopita kwa mwaliko wa mfalme wa nchi hiyo Sultan Qaboos bin Said.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Yousuf bin Alawi amewahi kutamka wazi wazi kwamba, Israel inakubalika kuwa ni nchi katika Mashariki ya Kati. Oman na Israel ambazo hazina uhusiano wa kidiplomasia, katika miaka ya 1990 zilikubaliana kufungua ofisi za uwakilishi wa kibiashara, lakini mwaka 2000, serikali ya Muscat ikatangaza kuzifunga baada ya kuanza Intifadha ya Pili ya Palestina.