Duru mpya ya mazungumzo ya Astana kuhusu Syria kuanza tena
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54702-duru_mpya_ya_mazungumzo_ya_astana_kuhusu_syria_kuanza_tena
Duru mpya ya mazungumzo ya Astana kuhusu mgogoro wa Syria inatazamiwa kuanza mapema mwezi ujao wa Agosti huko Nur-Sultan mji mkuu wa Kazakhstan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2019 21:55 UTC
  • Duru mpya ya mazungumzo ya Astana kuhusu Syria kuanza tena

Duru mpya ya mazungumzo ya Astana kuhusu mgogoro wa Syria inatazamiwa kuanza mapema mwezi ujao wa Agosti huko Nur-Sultan mji mkuu wa Kazakhstan.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Mikhail Bogdanov ambaye pia ni Mjumbe Maalumu wa Rais wa Russia katika masuala ya Asia Magharibi na Afrika na kuongeza kuwa, mkutano huo wa mwezi ujao wa Astana utafuatiwa na kikao kingine kuhusu hali ya Syria kitakachofanyika nchini Uturuki.

Amesema wawakilishi wa Lebanon na Iraq watashiriki mkutano huo wa kimataifa wa Astana kwa mara ya kwanza. Astana ni jina la zamani la mji mkuu wa Kazakhstan ambao kuanzia Machi mwaka huu ulibadilishwa jina na kuwa Nur-Sultan kwa ajili ya kumuenzi Nur-Sultan Nazarbayev, Rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu.

Miongoni mwa maudhui zitakazojadiliwa katika mazungumzo hayo ya Astana na kikao cha Uturuki kuhusu mgogoro wa Syria ni hali ya mambo katika mji wa Idlib, kadhia ya wakimbizi, hali ya kibinadamu na hatua zilizopigwa na Kamati ya Katiba. 

Kikao cha Astana nchini Kazakhstan

Aprili mwaka huu, duru ya 12 ya mazungumzo ya Astana kuhusiana na mgogoro wa Syria ilifanyika huko Nur-Sultan, mji mkuu wa Kazakhstan, ambapo wapinzani wa Syria, timu ya serikali ya Damascus, wawakilishi wa Iran, Russia na Uturuki walishiriki katika mkutano huo. 

Mazungumzo ya Astana yalianza Januari 2017 kwa ubunifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ushirikiano wa Russia na Uturuki kwa shabaha ya kurejesha amani na uthabiti nchini Syria.