Madai ya upotoshaji ya Trump kwamba Asia Magharibi imestawishwa na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56886-madai_ya_upotoshaji_ya_trump_kwamba_asia_magharibi_imestawishwa_na_marekani
Baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001 na kupitia kisingizio cha kupambana na ugaidi, Marekani ilianzisha hujuma zake dhidi ya eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ambapo mwaka 2001 Washington iliivamia kijeshi Afghanistan, huku mwaka 2003 ikiishambulia Iraq.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 27, 2019 04:44 UTC
  • Madai ya upotoshaji ya Trump kwamba Asia Magharibi imestawishwa na Marekani

Baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001 na kupitia kisingizio cha kupambana na ugaidi, Marekani ilianzisha hujuma zake dhidi ya eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ambapo mwaka 2001 Washington iliivamia kijeshi Afghanistan, huku mwaka 2003 ikiishambulia Iraq.

Baada ya hujuma hizo pia Washington iliingilia masuala ya ndani ya nchi za eneo hili hususan nchini Syria kwa lengo la kutekeleza mipango yake michafu. Hatua hizo za Marekani hazikuwa na matokeo mengine ghairi ya kusababisha mauaji ya halaiki na uharibifu mkubwa katika eneo. Pamoja na hayo, Rais Trump mwenye vituko na ambaye amepata umashuhuri kwa kusema uongo, amekosoa gharama zilizotolewa na serikali zilizotangulia za Marekani katika eneo la Asia Magharibi na kudai kuwa gharama hizo zimepelekea kufungwa viwanda vya nchi hiyo. Katika matamshi aliyoyatoa katika kituo cha Uadilifu wa Vyama Viwili jimboni Carolina Kusini Trump alisema: "Serikali za huko nyuma za Marekani zilimwaga kiasi cha Dola trilioni nane katika vita eneo la Asia Magharibi, siasa ambazo zilisaidia kujenga miji na nchi nyingine, huku zikiharibu miji mbalimbali ya Marekani. Hii ni katika hali ambayo gharama za mwaka mmoja za vita Asia ya Magharibi zingetuwezesha kudhamini msaada wa masomo kwa watoto wote wa Marekani, na bado tungesalia na kiasi kikubwa cha fedha za ziada. Hata hivyo vipindi hivyo vimefika ukingoni." Madai hayo ya Trump yanakinzana kikamilifu na uhalisia wa mambo. Trump ambaye kama ilivyo kawaida yake ya kusema uongo, anajaribu kuwahadaa watu kuhusu suala hilo. Ni wazi kuwa hali mbaya ya sasa nchini Afghanistani na Iraq imetokana na uwepo wa kijeshi wa Marekani katika nchi hizo.

Mauaji na jinai za kutisha, matokeo ya uvamizi wa Marekani Asia Magharibi

Hii ni kusema kuwa, uvamizi wa nchi hizo na serikali za huko nyuma za Marekani na hata baada ya hapo, si tu kwamba umepelekea makumi ya maelfu ya watu kuuawa, bali umepelekea pia kuharibiwa miundombinu na taasisi muhimu za viwanda, kilimo na huduma za kijamii. Kwa upande mwingine ni kwamba ikiongoza muungano wa nchi za Magharibi na Kiarabu, Washington imeingilia pia nchini Syria ambapo kupitia uungaji mkono wa kila upande kwa makundi ya kigaidi kwa lengo la kutaka kuiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo, imeitwisha serikali ya Damascus vita vya ndani, vyenye maafa na uharibifu mkubwa. Vita hivyo si tu kwamba vimepelekea malaki ya raia wa nchi hiyo kuuawa, bali vimeisababishia Syria hasara ya mamia ya mabilioni ya Dola kwenye sekta za miundombinu, miji mbalimbali na hata vijiji vya nchi hiyo ya Kiarabu. Huku Trump akidai kila mara kuwa serikali yake imeazimia kuwarejesha nyumbani askari wa Marekani wanaohudumu nje ya nchi, hivi sasa ametoa amri ya kuendelea kuhudumu askari laki mbili wa Marekani katika maeneo tofauti ya dunia.

Hali ilivyo Afghanistan, licha ya Trump kudai kuwa uvamizi wa Marekani umeijenga Asia Magharibi

Kinyume na ahadi yake ya kuondoka askari wa Marekani Asia Magharibi, kivitendo si tu kwamba katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni Trump hajachukua hatua yoyote katika uwanja huo, bali hivi karibuni ametuma askari elfu tatu wapya kwenda Saudi Arabia. Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, katika kipindi cha utawala wa Trump askari wengi zaidi wamepelekwa Asia Magharibi, kuliko kipindi cha Barack Obama. Katika hotuba zake rais huyo amekuwa akiwaambia Wamarekani kwamba, atahitimisha vita visivyo na mwisho, kama vile vya Afghanistan. Hata hivyo kinyume na madai hayo, Trump hajahitimisha vita vyovyote vile katika utawala wake, bali ametuma askari zaidi eneo la Asia Magharibi. Kuhusiana na suala hilo, gazeti la New York Times limeandika: "Trump hapendelei hata kidogo kuhitimisha vita, na badala yake anatuma askari kutoka sehemu moja kwenda nyingine." Ukweli ni kwamba Trump si tu kwamba hataki kuondoa askari wa nchi yake Asia Magharibi, bali kwa mtazamo wake, serikali tegemezi za eneo kama vile Saudi Arabia ni sawa na mfuko wa fedha ulio na faida kubwa za kiuchumi na kifedha kwa Marekani kupatia mauzo ya silaha na kuwekeana mikataba tofauti ya kibiashara na kiuchumi na serikali hizo.