Rais Bashar Al Assad: Yumkini Marekani haijamuua Baghdadi, bali imemficha
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i57199-rais_bashar_al_assad_yumkini_marekani_haijamuua_baghdadi_bali_imemficha
Rais Bashar al-Assad wa Syria ametilia shaka madai ya Marekani kuwa imemuua kinara wa kundi la kigaidi la Daesh, Abu Bakr Baghdadi, na kusisitiza kwamba huenda kiongozi huyo wa ISIS amejificha au amefichwa sehemu fulani na serikali ya Washington.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 11, 2019 07:50 UTC
  • Rais Bashar Al Assad: Yumkini Marekani haijamuua Baghdadi, bali imemficha

Rais Bashar al-Assad wa Syria ametilia shaka madai ya Marekani kuwa imemuua kinara wa kundi la kigaidi la Daesh, Abu Bakr Baghdadi, na kusisitiza kwamba huenda kiongozi huyo wa ISIS amejificha au amefichwa sehemu fulani na serikali ya Washington.

Assad amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Russia Today na kuongeza kuwa, "Operesheni ya kumuua Baghdadi ni njozi isiyo na tofauti na filamu za Hollywood, haifanani hata na masuala ya sayansi, bali ni mambo yasiyokuwa na ukweli wowote."

Rais wa Syria amesema yumkini Baghadadi ametekwa, amefichwa sehemu au uso wake umebadilishwa kwa njia ya upasuaji. Siku chache zilizopita, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kwamba kinara huyo wa (ISIS) ameuawa katika operesheni maalumu iliyofanywa na askari wa nchi hiyo huko katika mkoa wa Idlib, nchini Syria.

Amesema si rahisi kuamini mengi yaliyosemwa na Marekani kuhusiana na madai ya kuuawa kinara wa kundi la Daesh kutokana na nchi hiyo kuyaunga mkono magenge ya kigaidi nchini Syria.

Baghdadi, kinara wa ISIS ambaye Marekani inadai imemuangamiza

Kwingineko katika mahojiano hayo na televisheni ya Russia Today, Rais Bashar al-Assad wa Syria amekosoa vikali ubeberu wa Marekani na kusema kuwa, "Kama nchi nyingine za Magharibi, Marekani itapigana na taifa lolote lisilokubaliana nayo hata kama ni muitifaki. Itapigana na Russia, Iran na hata Syria madhali wanapinga ubeberu wao."

Kadhalika amekosoa operesheni ya kijeshi ya Uturuki dhidi ya nchi hiyo na kubainisha kuwa, "Wao (Waturuki) hawana tofauti na Israel ikija katika suala la ukaliaji ardhi kwa mabavu. Tofauti iliyopo ni kuwa sisi hatutambui uhalali wa uwepo wa dola hilo la Kizayuni."