Hamas yakosoa hatua ya Imarati kuialika Israel katika Maonyesho ya Dubai
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesema hatua ya Umoja wa Falme za Kiarabu ya kuualika utawala haramu wa Israel kushiriki katika Maonyesho ya Dubai ya 2020 ni aina fulani ya kuufanya wa kawaida uhusiano wa taifa hilo la Kiarabu na Tel Aviv.
Msemaji wa Hamas, Hazem Qassem amesema tabia kama hii ya kujipendekeza kwa Wazayuni inaupa kiburi utawala ghasibu wa Israel cha kushadidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina sanjari na kuendelea kuyavunjia heshimu matukufu ya ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu.
Baada ya kupokea mwaliko wa kushiriki maonyesho hayo ya kibiashara, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu alisema katika taarifa kuwa, "tunawapongeza waandalizi wa maonyesho hayo kwa kuialika Israel, tunakaribisha kwa mikono miwili ushiriki wa Israel katika maonyesho hayo ya Dubai."
Waandalizi wa maonyesho hayo ya kibiashara na ubunifu wamesema nchi 192 zimealikwa kushiriki maonyesho hayo, na kwamba utawala haramu wa Israel utashiriki pia.
Maonyesho hayo ya kibiashara ya Dubai Expo 2020 yanatazamiwa kufanyika kuanzia Oktoba 20 mwaka huu hadi Aprili 20 mwaka ujao wa 2021.
Baadhi ya nchi za Kiarabu zimekuwa zikifanya juu chini kuboresha uhusiano na utawala khabithi wa Kizayuni unaoukalia kwa mabavu mji wa Quds, kilipo kibla cha kwanza cha Waislamu duniani.