Syria: Ugaidi wa kiuchumi ni mwendelezo wa ugaidi wa kifizikia
Mwakilishi wa Kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa ugaidi wa kiuchumi ni mwendelezo wa hatua zilizo dhidi ya ubinaadamu za kuyatumia makundi ya kigaidi.
Bashar Jaafari ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akizungumzia suala la hali ya kibinaadamu nchini Syria na kuongeza kuwa, ugaidi wa kiuchumi unaotekelezwa na nchi za Magharibi dhidi ya serikali ya Damascus, ni mwendelezo wa hatua za kuyaunga mkono makundi ya kigaidi ambayo yamo katika orodha nyeusi ya Baraza la Usalama la Umoja huo. Mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa amebainisha kwamba serikali ya Damascus inashangazwa mno na kimya cha baadhi ya viongozi wa asasi za kimataifa kuhusiana na matatizo yanayowapata Wasyria yanayotokana na ugaidi, ubakaji na hatua mbovu za kiuchumi za upande mmoja pamoja na hatua za uvamizi za askari wa kigeni ndani ya taifa hilo la Kiarabu.
Kadhalika Bashar Jaafari sambamba na kubainisha kwamba Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imepuuza ripoti 64 zinazohusiana na hatua za uchumi wa kulazimishwa kwenye maisha ya mamilioni ya wananchi wa Syria, ameongeza kwamba, ofisi hiyo pia inajiepusha kuwafikishia misaada wakazi wa zaidi ya miji 40 iliyokombolewa kutoka mikononi mwa magaidi katika mkoa wa Idlib na viunga vyake. Mwakilishi wa Kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa pia amesisitiza ulazima wa kukomeshwa hatua mbovu za kiuchumi dhidi ya serikali ya Damascus na kuongeza kuwa, licha ya mashinikizo mengi dhidi ya raia wa nchi hiyo, lakini kamwe Syria haitofumbia macho haki yake ya kujitawala.