Imarati yazidi kuikumbatia Israel, yaruhusu ndege za utawala huo
Umoja wa Falme za Kiarabu umebatilisha sheria ya kuususia utawala haramu wa Israel na adhabu ya kukiuka sheria hiyo iliyokuwa imepiga marufuku kufanya miamala yoyote ya kibiashara na kifedha na utawala huo wa Kizayuni.
Hayo yametangazwa na shirika rasmi la habari la Imarati (WAM) na kuongeza kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa UAE, Sheikh Abdullah bin Zayed Al-Nahyan jana Jumamosi alisaini dikrii inayolenga kufuta Sheria ya Federali Nambari 15 ya Mwaka 1972, inayohusu kususiwa utawala haramu wa Israel na adhabu ya kukiuka sheria hiyo.
Shirika hilo la habari limefafanua kuwa, baada ya kusainiwa dikrii hiyo, "sasa inaruhusiwa kuingiza, kubadilishana au kumiliki bidhaa zote za Israel, sambamba na kufanya biashara (na Wazayuni)."
Wakati huo huo, safari ya kwanza ya anga ya moja kwa moja kati ya Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv na Abu Dhabi nchini Imarati inatazamiwa kufanyika Jumatatu ya kesho.
Duru za habari zinaarifu kuwa, ndege ya utawala wa Kizayuni itakayobeba wajumbe wa Israel na wapambe wa karibu wa Rais Donald Trump wa Marekani akiwemo mshauri wake, Jared Kushner itatua mjini Abu Dhabi Jumatatu.
UAE na utawala wa Kizayuni tarehe 13 mwezi huu zilifikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia kati yao. Mapatano hayo yaliyofikiwa kufuatia mashinikizo ya Marekani yamelaaniwa vikali katika kona mbalimbali za dunia.