Watoto 170 wa Palestina wamefungwa jela huko Israel mwaka 2020
Kamati ya Masuala ya Matekani wa Palestina imetangaza kuwa, watoto 170 wa Kipalestina walifungwa katika jela za utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 2020.
Taarifa iliyotolewa na kamati hiyo imesema kuwa, idadi ya matekani wa Kipalestina katika jela za Israel katika mwaka uliomalizika jana wa 2020 ilifikia watu 4,400; 170 kati yao ni watoto na 40 ni wanawake.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mwaka 2020 askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliwatia nguvuni Wapalestina 4,634 wakiwemo watoto 543 na wanawake 128.
Vilevile katika mwaka uliomalizika jana wa 2020 mahakama za Israel ziliwahukumu kifungo cha maisha Wapalestina wengine 5 na kuifanya idadi ya Wapalestina waliohukumiwa kifungo cha maisha katika mahakama hizo kufikia 543.
Ripoti ya Kamati ya Masuala ya Matekani wa Palestina imesema kuwa, wateka 700 wa Kipalestina wanasumbuliwa na maradhi katika jela za Israel na wanahitajia uangalizi na huduma za kitiba. Mateka wengine 140 wa Kipalestina wamepatwa na maradhi ya corona.
Siku chache zilizopita Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mohammad Shtayyeh aliuokosoa vikali utawala haramu wa Israel kwa uamuzi wake wa kukataa kuwapa chanjo mateka wa Palestina wanaoshikiliwa katika korokoro za utawala huo.