Mar 19, 2021 02:44 UTC
  • Makundi ya Palestina yasisitiza kufanyika uchaguzi na kuunda chombo kimoja cha uongozi

Makundi ya Palestina yametoa taarifa mwishoni mwa kikao chao huko Cairo mji mkuu wa Misri yakikisisitizia kufanyika uchaguzi na kuunda chombo kimoja cha uongozi.

Shirika la habari la "Falastin al Yaum" limeripoti kuwa, makundi hayo ya Palestina Jumatano wiki hii baada ya kumalizika vikao vyao vya siku mbili huko Cairo vilitoa taarifa;  ambapo yalisisitizia wajibu wa kulindwa umoja wa kisheria na kisiasa wa ardhi za Palestina na ulazima wa kufanyika uchaguzi huko Quds, Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza na kukabiliana na ukwamishaji wa aina yoyote wa utawala wa Kizayuni katika uwanja huo.  

Image Caption

Taarifa  hiyo imeongeza kuwa, duru hii ya mazungumzo imefanyika kwa lengo la kuondoa vizuizi katika njia ya kuelekea uchaguzi wa bunge na pia kutatua baadhi ya hitilafu zilizopo.  

Vikao vya viongozi wa makundi ya Palestina vinatazamiwa kuendelea ili kufuatilia yale yote yaliyokubaliwa katika duru ya kikao cha karibuni huko Cairo. 

Uchaguzi wa bunge wa Palestina umepangwa kufanyika tarehe 22 mwezi Mei mwaka huu, uchaguzi wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina tarehe 31 mwezi Julai na ule wa baraza la Taifa la Palestina tarehe 31 Agosti mwaka huu. 

Tags