Sababu na radiamali za kuakhirishwa uchaguzi wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i69644-sababu_na_radiamali_za_kuakhirishwa_uchaguzi_wa_palestina
Hatua ya Rais Muhmous Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kuakhirisha uchaguzi wa nchi hiyo imekabiliwa na radiamali tofauti za makundi ya kisiasa ya Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 01, 2021 10:20 UTC

Hatua ya Rais Muhmous Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kuakhirisha uchaguzi wa nchi hiyo imekabiliwa na radiamali tofauti za makundi ya kisiasa ya Palestina.

Mahmoud Abbas Ijumaa asubuhi alitangaza rasmi uamuzi wake wa kuakhirisha kwa muda uchaguzi mkuu wa Palestina kwa hoja kuwa hakuna uwezekano wa kujumuishwa Quds Tukufu katika uchaguzi huo. Awali uchaguzi wa bunge la Palestina ulikuwa umepangwa ufanyike tarehe 22 Mei, wa rais tarehe 31 Julai na wa mabaraza ya miji tarehe 31 Agosti mwaka huu.

Mahmoud Abbas amedai kuwa uamuzi wa utawala ghasibu wa Israel wa kutoruhusu uchaguzi umefanyike katika eneo la Quds inayokaliwa kwa mabavu ndiyo sababu ambayo imempelekea achukue uamuzi wa kuakhirisha kwa muda uchaguzi huo. Katika kipindi cha wiki chache zilizopita utawala huo umetoa mashinikizo makubwa dhidi ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ili ifutile mbali uchaguzi huo moja kwa moja. Israel unalichukulia eneo hilo kuwa sehemu ya ardhi inazozikalia kwa mabavu. Disemba 2017, serikali ya Donald Trump rais wa zamani wa Marekani ilichukuwa hatua iliyo kinyume cha sheria za kimataifa ya kuutambua mji wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Israel na hatimaye kuamua kuuhamishia ubalozi wake katika mji huo kutoka mjini Tel Aviv Mei 2018. Hatua hiyo iliufanya utawala huo ghasibu umee pembe na kuingiwa na tamaa ya kutaka kuudhibiti mji mzima wa Quds.

Mji mtakatifu wa Quds

Hata kama Mahmoud Abbas ametumia hatua ya tawala wa Israel ya kutoruhusu kufanyika uchaguzi katika eneo hilo kuwa kisingizio kizuri cha kuakhirisha uchaguzi Palestina nzima, lakini ni wazi kuwa wasi wasi wake wa kushindwa katika uchaguzi umechangia pakubwa katika uamuazi wake huo. Wataalamu wa Mambo wanaamini kuwa upinzani wa Israel wa kufanyika uchaguzi katika eneo la Beitul Muqaddas Mashariki ni kisingizio tu ambacho kimetumiwa na Abbas kuakhirisha uchaguzi ambapo kumekuwa na uwezekano mkubwa wa yeye kushindwa na makundi ya Kiislamu.

Mara tu baada ya kutangazwa tarehe ya uchaguzi, mrengo wa Fat'h ambapo Abbas ni mmoja wa viongozi wake, uligawanyika katika makundi kadhaa. Wanachama wanaompinga Mahmoud Abbas waliamua kuwasilisha majina ya wagombea wao na hivyo kudhoofisha nafasi ya ushindi kwa wagombea rasmi wa mrengo huo. Kwa msingi huo ilitarajiwa tangu awali kwamba Abbas angetumia kisingizio cha Israel kukataa kuruhusu kufanyika uchaguzi huko Quds, kama fursa nzuri ya kuakhirisha uchaguzi mzima ili kukwepa fedheha ya kushindwa katika uchaguzi huo.

Uamuzi wake huo umekabiliwa na radiamali kali na kubwa ndani ya Palestina. Chama cha Mapambano ya Kiislamu Hamas, kimetoa taarifa kikisema kwamba chama cha Fat'h na Mamlaka ya Ndani ya Palestina ndio watakaobeba dhima ya matokeo ya uamuzi huo wa Abbas ambao umetajwa kuwa 'mapinduzi dhidi ya mwenendo wa kushirikishwa makundi ya Palestina na mapatano ya kitaifa.' Hamas imeashiria kikoa kilichofanyika Ramallah Alkhamisi usiku na kusema kuwa ilisusia kikao hicho kwa sababu tayari ilikuwa imejua uamauzi ambao ulikuwa umepangwa kutangazwa rasmi na kwamba uamuazi huo ulitokana na masuala mengine ambayo hayana uhusiano wowote na Quds. Kwa maneno mengine ni kwamba Hamas inaamini kuwa wasi wasi wa Fath kushindwa kwenye uchaguzi kama ilivyokuwa hali katika uchaguzi wa 2006 ndio sababu kuu ambayo imempelekea Abbas aakhirishe uchaguzi huo.

Hamas

Radiamali nyingine kuhusu suala hilo imetolewa na kamati za mapambano za watu wa Palestina ambazo zimetaka kufutiliwa mbali mapatano ya Oslo na utawala ghasibu wa Israel, suala ambalo ni wazi kuwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina katu haitalikubali. Hii ni kwa sababu kabla ya hapo pia mamlaka hiyo haikuchukua hatua yoyote dhidi ya utawala wa Israel kufuatia kutekelezwa mapatano ya hiana ya 'Muamala wa Karne'. Msemaji wa kamati hizo amesema kwamba tatizo kuu la Palestina ni Oslo na mapatano mengine ya fedheha ambayo yamewafanya Wapalestina kuwa mateka. Amesisitiza kwamba mapatano ya Oslo na mengine kama hayo yanapasa kufutiliwa mbali na Mamlaka ya Ndani ya Palestina na pia  mamlaka hiyo kufutilia mbali uamuzi wake wa kuutambaua rasmi utawala ghasibu wa Israel.