Leo Wapalestina wanafanya maandamano makubwa ya kupinga Uzayuni
Vijana wa Palestina wametangaza kuwa, leo Ijumaa watafanya maandamano makubwa katika kona zote za Palestina, maandamano ambayo yatapewa jina la "Mapambazuko."
Mtandao wa habari wa Arabi 21 uliripoti habari hiyo jana na kuongeza kuwa, kutokana na wanajeshi makatili wa Israel kuendelea kuwanyanyasa na kuwakandamiza Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, vijana wa taifa hilo wametangaza maandamano makubwa ya maeneo yote ya Palestina leo Ijumaa.
Ikumbukwe kuwa jana walowezi wa Kizayuni waliuvamia tena Msikiti wa al Aqsa kwa msaada kamili wa wanajeshi dhalimu wa Israel.
Katika kujibu uvamizi na jinai hizo, vijana wa Palestina wametangaza kuwa, leo Ijumaa wataanzisha harakati kubwa itakayopewa jina la "Mapambazuko" na itafanyika katika ardhi zote za Palestina.
Lengo la vijana hao ni kupanua wigo wa mapambano ya taifa la Palestina dhidi ya utawala ghasibu na katili wa Kizayuni.
Licha ya kwamba tarehe 31 Mei, utawala wa Kizayuni uliomba kusitishwa mapigano baina yake na makundi ya muqawama ya Palestina, lakini wanajeshi dhalimu wa Israel wanaendelea kuwakandamiza na kuwanyanyasa Wapalestina wa maeneo tofauti.
Wanamapambano wa Palestina ikiwemo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS wameuonya tena utawala wa Kizayuni usiendelee kuwanyanyasa Wapalestina na kusema kuwa, wanamuqawama hao ikiwemo HAMAS hivi sasa wana uwezo wa kuvurumisha mamia ya makombora kwa kila dakika moja na kupiga maeneo ya Wazayuni.
Kiongozi wa HAMAS katika Ukanda wa Ghaza, Yahya Sinwar alisema juz Jumatano mbele ya waandishi wa habari mjini Ghaza kuwa: Muqawama uliodhihirishwa hivi karibuni wakati wa kuihami Ghaza, ni sehemu ndogo kabisa ya uwezo wa HAMAS.