Hamas yaghadhabishwa na Google, Apple kuiondoa 'Palestina' katika ramani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71864-hamas_yaghadhabishwa_na_google_apple_kuiondoa_'palestina'_katika_ramani
Ofisi ya Habari ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imekosoa vikali hatua ya mashirika ya Kimarekani ya Google na Apple ya kuliondoa neno 'Palestina' katika ramani zao za dunia. Kwa mujibu wa mashirika hayo, hivi sasa hakuna pahala duniani panapotambulika kama Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 01, 2021 03:10 UTC
  • Hamas yaghadhabishwa na Google, Apple kuiondoa 'Palestina' katika ramani

Ofisi ya Habari ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imekosoa vikali hatua ya mashirika ya Kimarekani ya Google na Apple ya kuliondoa neno 'Palestina' katika ramani zao za dunia. Kwa mujibu wa mashirika hayo, hivi sasa hakuna pahala duniani panapotambulika kama Palestina.

Taarifa ya Ofisi ya Habari ya Hamas imebainisha kuwa, kwa mara nyingine tena, mashirika ya Google na Apple yamefuta kabisa athari za kihistoria na kisheria za Wapalestina, kwa kitendo hicho cha kifidhuli cha kuiondoa Palestina katika ramani zake za dunia.

Ofisi ya Habari ya harakati hiyo ya muqawama imeeleza kuwa, kitendo hicho cha Google na Apple ni cha kiudui na kiuhasama dhidi ya wananchi wa Palestina na haki zao, na pia kinakiuka hati na maazimio ya kimataifa.

Julai mwaka jana pia, shirika la Kimarekani la Google mbali na kuondoa neno Palestina katika ramani zake zote za dunia, lakini pia liliyaarifisha maeneo mawili ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, kama sehemu za Israel.

Google na Apple zinavyoihujumu Palestina

Maelfu ya watumiaji wa mitandao ya kijamii ndani na nje ya Palestina walighadhabishwa mno na kitendo hicho cha kiuadui, kilichofanywa kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wizara ya Utalii ya utawala wa Kizayuni wa Israel imewahi kuchapisha pia ramani mpya ya mji wa Quds tukufu ambayo ndani yake maeneo yote matakatifu ya Kiislamu na Kikristo yamefutwa.

Wapalestina wanasisitiza kuwa, vitendo hivyo vya Wazayuni na Wamarekani vinakusudia kuyayahudisha maeneo matukufu ya dini za Kiislamu na Kikristo yenye historia ndefu sambamba na kupotosha utambulisho wa maeneo hayo.