Katibu Mkuu wa UN atahadharisha kuenea kwa harakati za Daesh duniani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i724-katibu_mkuu_wa_un_atahadharisha_kuenea_kwa_harakati_za_daesh_duniani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, hadi mwishoni mwa mwaka uliopita makundi zaidi ya 30 ya kigaidi yalitangaza utiifu wao wa kushirikiana na kundi la kitakfiri la Daesh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2016 11:32 UTC
  • UN Secretary General
    UN Secretary General

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, hadi mwishoni mwa mwaka uliopita makundi zaidi ya 30 ya kigaidi yalitangaza utiifu wao wa kushirikiana na kundi la kitakfiri la Daesh.

Ban Ki-moon amesema Daesh ni "tishio lisilo na mfano" kwa sababu kundi hilo la kigaidi lina uwezo wa kuyavuta makundi mengine ya kigaidi katika nchi kama Ufilipino, Uzbekistan, Pakistan, Libya na Nigeria.

Ban amekadiria kuwa makundi ya kigaidi yanayounga mkono Daesh yataongezeka katika kipindi cha mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa nchi zote zinapaswa kujiweka tayari kukabiliana na ongezeko la mashambulio ya kigaidi ya Daesh na makundi yenye mfungamano na kundi hilo la kigaidi na kitakfiri.

Ban amesema:"kupanuka hivi karibuni ushawishi wa Daesh katika maeneo yote ya Magharibi na Kaskazini mwa Afrika, Mashariki ya Kati, Kusini na Kusini Mashariki mwa Asia kunadhihirisha kasi ya kuongezeka kitisho hicho na jinsi kilivyojizatiti duniani kote katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelitaja Daesh kuwa "kundi tajiri zaidi la kigaidi duniani" na kuongeza kuwa licha ya vikwazo vyote lilivyowekewa, katika mwaka uliopita pato la kundi hilo la kigaidi lililotokana na mauzo ya mafuta na bidhaa nyengine zinazotokana nayo lilikuwa ni baina ya dola milioni 400 hadi 500.../