Daesh wamalizana wenyewe kwa wenyewe, 50 wauawa Damascus
Makumi ya wachama wa makundi ya kigaidi wameuawa kutokana na kushamiri malumbano miongoni mwao huko Damascus, mji mkuu wa Syria.
Habari zinasema kuwa, wanachama 50 wa makundi hayo wameuawa kutokana na uhasama juu ya eneo ambalo liko chini ya udhibiti wao viungani mwa Damascus.
Habari zaidi zinasema kuwa, kundi la kigaidi la Jaishul Islam linaloungwa mkono wa Saudi Arabia limekabiliana vikali na kundi jingine la Faylaq al-Rahman, ambalo ni tawi la kundi la al-Nusra, lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda katika eneo la Ghouta, mashariki mwa Damascus.
Hii ni katika hali ambayo, jeshi la Syria linaendelea na mapambano yake dhidi ya magenge hayo ya kigaidi yanayoungwa mkono na madola ya kigeni. Wiki iliyopita, duru za habari ziliripoti habari ya kuangamizwa zaidi ya magaidi 300 katika mapigano baina ya genge la kigaidi la Jaishul Islam na magenge mengine yenye silaha katika eneo la Ghuta Mashariki, kusini mwa Damascus, mji mkuu wa Syria. Mauaji mapya ya magaidi yamepelekea idadi ya waliouawa hadi sasa tokea mwezi uliopita wa Aprili kutokana na malumbano na uhasama wa wenyewe kwa wenyewe kufikia watu 500.
Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 baada ya magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani na waitifaki wake kuanzisha mashambulizi ya kinyama dhidi ya raia na maafisa wa serikali ya Syria kwa nia ya kutaka kuipindua serikali halali ya Rais Bashar al Assad wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu zaidi ya laki nne wameuawa tokea nchi hiyo iingie kwenye mgogoro mwaka 2011.