UN: Jeshi la Israel limeua Wapalestina 59 Ukingo wa Magharibi
Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibinadamu Kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) limesema jeshi la Israel limeua Wapalestina 59 katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu ndani ya mwaka huu 2021 pekee.
Katika taarifa, UNRWA imesema: Mwaka 2021 pekee, Vikosi vya Ulinzi vya Israel (ISF) vimeua Wapalestina 59 katika Ufukwe wa Magharibi, wakiwemo wakimbizi 22 na watoto 13.
Taarifa ya taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, wananchi 984 wa Palestina wamejeruhiwa kwa risasi hai za jeshi la Israel katika kipindi hicho cha miezi saba ya kwanza ya mwaka huu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibinadamu kwa Wakimbizi wa Palestina limeutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ufanye uchunguzi juu ya mauaji hayo, na kuwafikisha mbele ya sheria waliohusika.
Kadhalika UNRWA imelaani mauaji ya Imad Saleh Khaled Hashash, mkimbizi kutoka kambi ya Balata, aliyeuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel Jumanne iliyopita katika Ukingo wa Magharibi.
Ripoti zinaeleza kuwa, kijana huyo wa miaka 15 aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Wavulana ya Balata aliuawa kwa risasi alipokuwa amesimama juu ya paa la nyumba yao.