Russia: Marekan inawahamishia Afghanistan magaidi wa Daesh
Naibu Kamanda wa Wilaya ya Kati ya Jeshi la Russia amesema kuwa jeshi la Marekani linawahamisha magaidi walioko Syria na kuwapeleka Afghanistan.
Rostam Minkayev amesema kuwa, Moscow inazo taarifa zinazothibitisha kuwa Marekani inahamisha wapiganaji wa makundi ya kigaidi likiwemo kundi la Daesh kutoka maeneo yanayodhibitiwa na nchi hiyo huko kaskazini mwa Syria na kuwapeleka nchini Afghanistan.
Marekani iliondoa majeshi yake nchini Afghanistan mwezi uliopita wa Septemba baada ya kundi la Taliban kudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul. Hata hivyo hadi sasa hakuna nchi iliyotambua rasmi serikali ya kundi la Taliban, na jamii ya kimataifa imetangaza kuwa, haina haraka katika suala hilo.

Mafanikio ya kundi la Taliban ya kuudhibiti mji wa Kabul yalihitimisha miaka 20 ya uvamizi wa Marekani na washirika wake dhidi ya nchi ya Afghanistan.
Marekani iliivamia Afghanistan kwa kaulimbiu ya kuimarisha demokrasia na haki za binadamu. Hata hivyo takwimu zinaonesha kuwa, uvamizi huo wa Marekani haukuwa na matunda yoyote ghairi ya kuzidisha machafuko, uzalisha wa madawa ya kulevya, uharibifu na mauaji ya maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan.