Jeshi la Iraq laendelea kushirikiana na al Hashd al Shaabi kupambana na magaidi
(last modified 2021-10-26T12:15:43+00:00 )
Oct 26, 2021 12:15 UTC
  • Jeshi la Iraq laendelea kushirikiana na al Hashd al Shaabi kupambana na magaidi

Vikosi mbalimbali vya jeshi la Iraq vinaendelea kushirikiana na harakati ya kujitolea ya wananchi wa nchi hiyo maarufu kwa jina la al Hashd al Shaabi kupambana na magaidi kusini mwa mji wa Mosul, kaskazini mwa Iraq.

Kwa mujibu wa Alsumaria News, operesheni ya pamoja na jeshi na harakati kujitolea ya wananchi wa nchi hiyo, al Hashd al Shaabi imeendelea pia leo Jumanne katika jangwa la al Hadhar kusini mwa mji wa Mosul katika mkoa wa Nainawa (Nineve) kaskazini mwa Iraq kwa shabaha ya kusafisha mabaki ya magaidi wakufurishaji.

Siku chache zilizopita pia, askari wa al Hashd al Shaabi walifanya opesheni kali ya kusafisha magaidi mkoani Baghdad na kufanikiwa pamoja na mambo mengine, kugudundua maficho ya kiognozi mmoja wa ngazi za juu wa magaidi wa Daesh (ISIS) na kumtia mbaroni.

Licha ya kusambaratishwa magenge ya kigaidi huko Iraq, lakini mabaki ya magaidi hao waliojificha ndani ya jamii bado yapo. 

Harakati ya kujitolea ya wananchi wa Iraq, al Hashd al Shaabi

 

Mara kwa mara jeshi la Iraq kwa kushirikiana na harakati ya al Hashd al Shaabi linaendesha operesheni za kusafisha maeneo mbalimbali ya nchi hiyo hususan yale ya kaskazini.

Katikati ya mwezi huu wa Oktoba, Komandi ya Vikosi vya Gadi ya Mipakani ya Iraq ilitangaza kuwa hivi sasa jeshi la nchi hiyo linalidhibiti kikamilifu eneo la mpaka wa Iraq na Syria.

Hamid al Husseini Kamanda wa kikosi cha walinzi wa mpakani cha Iraq alitangaza kuwa, askari wa nchi hiyo wameimarisha ulinzi wa maeneo ya mpakani na tayari wamekamilisha kazi ya kuzungushia uzio na ujenzi wa minara katika ukanda mzima wa eneo la mpaka wa nchi hiyo na Syria.  

Tags