Viongozi wa Israel wakiri kushindwa katika vita vya mawasiliano ya Intaneti
Televisheni moja ya nchini Lebanon imetangaza kuwa, viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamekiri kwamba wameshindwa katika vita vya mawasiliano ya Intaneti (Cyber War) na hadi hivi sasa wameshindwa kujua namna ya kujihami katika vita hivyo.
Televisheni ya al Mayadeen ilitangaza hayo jana Jumatatu na kuwanukuu viongozi wa Israel wakikiri kwamba, hadi hivi sasa wameshindwa kujua mashambulio dhidi ya sekta zake nyeti na muhimu sana yamefanyika vipi na kwa nini wameshindwa kukabiliana nayo.
Kanali ya 13 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni wa Israel imetangaza kuwa, mashambulio ya Intaneti yaliyofanyika dhidi ya taasisi za Israel ni ya hatari sana. Imeongeza kuwa, mashambulio hayo dhidi taasisi nyeti za Israel zina udhaifu mkubwa kiasi kwamba zinashindwa kujihami.
Wiki iliyopita gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth liliandika kwamba, kundi moja lilidukua taarifa nyeti na za siri za jeshi la Israel na kuzisambaza mitandaoni. Taarifa hizo zilihusu habari za kina na za ndani za mamia ya wanajeshi na maafisa wa kijeshi wa Israel.
Siku chache baadaye gazeti jingine la Kizayuni la Jerusalem Post lilidai kuwa kundi la wadukuzi la Kiirani liitwalo "Kivuli Cheusi" ndilo lililofanya mashambulio hayo dhidi ya Cyberserver ya Israel na kuitoa kwenye udhibiti wa Wazayuni. Kundi hilo lilitishia kufichua na kuweka hadharani taarifa nyingine nyingi za siri zaidi kuhusu taasisi nyeti za utawala wa Kizayuni.
Baada ya kutolewa tishio hilo, muasisi na mkurugenzi wa shirika la CONFIDENCE ambalo linajihusisha na usalama wa mitandao ya Intaneti alisema kuwa, kama taarifa za siri za Israel zitatangazwa hadharani, basi mfumo wa usalama wa utawala wa Kizayuni utapata hasara na pigo kubwa.
Wiki iliyopita pia, baadhi ya vituo vya kusambaza mafuta nchini Iran liliathiriwa na mashambulio ya Intaneti na serikali ya Iran inazituhumu Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ndizo zilizofanya mashambulio hayo.