Sheikh Qassim: Waislamu wakabaliane na mwenendo wa kuanzishwa uhusiano na Israel
Kiongozi wa Waislamu wa Kishia nchini Bahrain ametoa wito wa kusimama kidete Waislamu katika kukabiliana na mwenendo wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Sheikh Issa Qassim amesema hayo katika hafla ya kumbukumbu ya miaka 11 tangu kuanza harakati za wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa Kifamilia wa Aal Khalifa na kusisitiza kwamba, kuna haja ya Waislamu kusimama kidete kwa ajili ya kukabiliana na mchakato wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel.
Bahrain, ambayo idadi kubwa ya wananchi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia inatawaliwa na utawala wa Kifalme wa aila ya Kisunni ambao umekubuhu katika ukiukaji wa haki za binadamu.
Utawala huo wa kiimla umekuwa ukikandamiza wapinzani tangu ulipotumia mkono wa chuma mwaka 2011 kwa msaada wa Saudi Arabia kupambana na maandamano ya umma ya kupigania mageuzi.
Mbali na adhabu za vifungo, utawala wa Aal Khalifa umewafutia uraia pia mamia ya Wabahrain katika kesi zilizoendeshwa kwa umati na mahakama za utawala huo.
Kwa mujibu wa taasisi za kutetea haki za binadamu, hukumu za adhabu ya kifo zimeongezeka mno pia nchini humo katika muongo mmoja uliopita hasa tangu lilipoanza vuguvugu la Machipuo ya Kiarabu mwaka 2011.
Asasi na jumuiya mbalimbali za haki za binadamu zimelaani mara chungu nzima ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Bahrain dhidi ya raia wa nchi hiyo wanaopaza sauti wakitaka mageuzi.