Syria yaitaka UN iibebeshe dhima Israel kwa jinai zake Golan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81806-syria_yaitaka_un_iibebeshe_dhima_israel_kwa_jinai_zake_golan
Mwakilishi wa Kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo liuwajibishe na kuubebesha dhima utawala wa Kizayuni wa Israel kwa jinai ulizozifanya katika Miinuko ya Golan ya Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 26, 2022 09:07 UTC
  • Syria yaitaka UN iibebeshe dhima Israel kwa jinai zake Golan

Mwakilishi wa Kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo liuwajibishe na kuubebesha dhima utawala wa Kizayuni wa Israel kwa jinai ulizozifanya katika Miinuko ya Golan ya Syria.

Hussam Eddin Ala alitoa mwito huo jana Ijumaa katika taarifa yake kwa kikao cha 49 cha Baraza la Haki za Binadamu na kuongeza kuwa, Israel inapaswa kuadhibiwa kwa jinai zake za kimfumo, kama kupora ardhi na rasilimali za Wasyria katika eneo la Golan.

Amesema jamii ya kimataifa inapaswa kukomesha mipango ya utawala pandikizi wa Israel ya kubadili sura ya mji, muundo wa jamii na hali ya kisheria ya eneo la Golan la Syria lililovamiwa na kukaliwa kwa mabavu, hususan ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika eneo hilo.

Eddin Ala amebainisha kuwa, ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala haramu wa Israel umewezidishia mashaka na matatizo si tu wakazi wa Golan ya Syria, bali wananchi madhulumu wa Palestina hususan katika mji wa Quds.

Miinuko ya Golan ya Syria

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Syria amekumbusha kuwa, eneo la Golan ni milki ya Syria na kwamba maazimio na sheria za kimataifa zinasisitiza suala hilo, na lazima eneo hilo lirejee chini ya mamlaka ya Syria. 

Umoja wa Mataifa umepasisha mara kadhaa azimio la kuitaka Israel kuondoka kikamilifu eneo la Golan la Syria na kurejea katika mpaka wa tarehe 4 Juni mwaka 1967.