Amir wa Qatar aikosoa dunia kwa kupuuza kughusubiwa ardhi za Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81848-amir_wa_qatar_aikosoa_dunia_kwa_kupuuza_kughusubiwa_ardhi_za_palestina
Amir wa Qatar amekosoa vikali hatua ya utawala ghasibu wa Israel ya kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kusisitiza kuwa, asilimia kubwa ya jamii ya kimataifa imefumbia macho kadhia hiyo kwa miongo kadhaa sasa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 27, 2022 10:50 UTC
  • Amir wa Qatar aikosoa dunia kwa kupuuza kughusubiwa ardhi za Palestina

Amir wa Qatar amekosoa vikali hatua ya utawala ghasibu wa Israel ya kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kusisitiza kuwa, asilimia kubwa ya jamii ya kimataifa imefumbia macho kadhia hiyo kwa miongo kadhaa sasa.

Tamim bin Hamad Aal-Thani alisema hayo jana Jumamosi katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa duru ya 20 ya Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Doha katika mji mkuu wa nchi hiyo na kueleza kuwa, "mamilioni ya Wapalestina wamenyongeka kutokana na Israel kughusubu ardhi zao, na jamii ya kimataifa kupuuza kadhia hiyo kwa miongo saba sasa."

Amesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa imeshindwa kuwatendea haki na uadilifu wananchi madhulumu wa Palestina, na watu wengine katika eneo la Asia Magharibi.

Tamim bin Hamad Aal-Thani amebainisha kuwa, madai ya chuki dhidi ya Mayahudi hivi sasa yanatumika vibaya dhidi ya mtu yoyote anayekosoa sera za Tel Aviv.

Mapema jana, Mohammad Shtayyeh, Waziri Mkuu wa Palestina alikutana na kufanya mazungumzo na Amir wa Qatar pambizoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Doha na kuishukuru nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi kwa kuwatetea Waplestina na kupigani haki zao.

Shtayyeh alisema: Israel kwa mpangilio maalumu inasambaratisha uwezekano wa kuundwa taifa la Palestina, kwa kushadidisha ujenzi wa vitongoji haramu, kupora ardhi na kubomoa nyumba za Wapalestina.