HRW: Polisi ya Misri inawakandamiza wakimbizi wa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81882-hrw_polisi_ya_misri_inawakandamiza_wakimbizi_wa_sudan
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeishutumu polisi kwa kuwazuilia kinyume cha sheria na kuwatesa makumi ya wakimbizi wa Sudan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 28, 2022 06:35 UTC
  • HRW: Polisi ya Misri inawakandamiza wakimbizi wa Sudan

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeishutumu polisi kwa kuwazuilia kinyume cha sheria na kuwatesa makumi ya wakimbizi wa Sudan.

Shirika hilo limesema jeshi la polisi la Misri limewatia mbaroni raia 30 wa Sudan wanaoishi kama wakimbizi au watafuta hifadhi nchini humo, na linawazuilia kinyume cha sheria mpaka sasa.

Taarifa ya Human Rights Watch imeeleza kuwa, wakimbizi hao wa Sudan wanafanyiwa kila aina ya mateso na udhalilishaji na askari polisi wa Misri, baadhi yao wakitumikishwa na kufanyishwa kazi za sulubu.

Joe Stork, afisa wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjin New York ameitaka Ofisi ya Mwendesha Mashitaka ya Umma kuchunguza na kuwafikisha mbele ya sheria maafisa usalama wanaotuhumiwa kuwakandamiza na kuwatesa wakimbizi wa Sudan.

Ukandamizaji Misri

Asasi za kiraia mjini Cairo zimesema makumi ya wakimbizi na raia hao wa Sudan wanaotafuta hifadhi nchini Misri walikamatwa katika operesheni iliyofanyika baina ya Disemba 27 na Januari 5, na wangali wanazuiliwa na kuteswa hadi sasa.

Katika miezi ya karibuni, asasi nyingi za kimataifa na za kutetea haki za binadamu zimetoa indhari kuhusu utendaji wa utawala wa Misri unaoongozwa na Rais Abdul Fattah al-Sisi katika masuala ya uhuru wa kijamii na kisiasa na ukiukaji wa haki za binadamu.