HAMAS: Muqawama ndiyo njia ya kimsingi zaidi ya kuihami Quds Tukufu
Mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, Baytul Muqaddas ndio mji mkuu wa milele wa Palestina na kusisitiza kuwa, kinachoifanya Quds ibakie ni kuendelezwa muqawama mbele ya adui vamizi.
Shirika la habari la Anadolu limemnukuu Osama Hamdan akisema hayo kwenye kongamano lililozungumzia matukio ya Palestina chini ya kivuli vya kutangazwa uhusiano wa kawaida na Israel kulikofanywa na baadhi ya nchi za Kiarabu. Kongamano hilo limefanyika mjini Rabbat, Morocco.
Amesisitiza kuwa, Baytul Muqaddas kamwe haiwezi kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, na kwamba kila Mpalestina ataendelea kusimama kidete kuilinda Quds. Mji wa Quds ndiko uliko Msikiti wa al Aqsa ambao ndicho Kibla cha Kwanza cha Waislamu.
Mji huo ni sehemu isiyotenganishika na ardhi ya Palestina na ni moja ya maeneo matatu matukufu zaidi kwa Waislamu ulimwenguni baada ya miji ya Makka na Madina.
Usama Hamdan pia amesema, mapambano makali yaliyotokea huko Quds katika siku za hivi karibuni ni ushahidi wa wazi kwamba Wapalestina kamwe hawawezi kuacha kuilinda Quds na Kibla cha Kwanza cha Waislamu.
Mbali na mapambano hayo kuwa majibu kwa uvamizi wa Wazayuni katika Msikiti wa al Aqsa, pia ni muendelezo usiosita wa kuulinda Msikiti wa al Aqsa. Amesema harakati hiyo ilipamba moto tangu rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump alipouhamishia mjini Quds ubalozi wa Marekani uliokuweko Tel Aviv.
Mwaka 2020 nchi za Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati), Bahrain, Morocco na Sudan ziliangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Kwa kujidhalilisha kwao hivyo kwa Wazayuni, nchi hizo nne za Kiarabu zilisaliti waziwazi kadhia muhimu zaidi ya umma wa Kiislamu, yaani kadhia ya Palestina na Quds.