Israel yaidhinisha Saudia kupewa visiwa viwili vya Misri
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i85914-israel_yaidhinisha_saudia_kupewa_visiwa_viwili_vya_misri
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeripotiwa kubariki mpango wa kukabidhi visiwa viwili vya kistratajia vya Misri kwa Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 15, 2022 22:12 UTC
  • Israel yaidhinisha Saudia kupewa visiwa viwili vya Misri

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeripotiwa kubariki mpango wa kukabidhi visiwa viwili vya kistratajia vya Misri kwa Saudi Arabia.

Shirika la habari la Axios limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, kwa miezi kadhaa sasa, Washington imekuwa ikisimamia kwa siri mazungumzo kuhusiana na mpango huo wa kukabidhiwa Riyadh visiwa vya Tiran na Sanafir, ambao ulizusha ghadhabu, malalamiko na maandamano nchini Misri.

Ripoti ya Axio imeeleza kuwa, makubaliano hayo yanatazamiwa kutangazwa rasmi mwishoni mwa wiki hii, katika safari ya Rais Joe Biden wa Marekani nchini Saudia.

Habari zaidi zinasema kuwa, mpango wa kukabidhi visiwa viwili vya kistratajia vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kwa Saudi Arabia utaandaa mazingira ya kuanzishwa rasmi uhusiano wa kawaida wa Riyadh na Tel Aviv.

Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, Mohammad Bin Salman

Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri na katika jitihada za kuboresha mahusiano kati ya Cairo na Riyadh aliamua kuiuzia Saudia visiwa vya Tiran na Sanafir mwaka 2016, hatua ambayo ilikabiliwa na malalamiko makubwa ya Wamisri.

Mazungumzo yaliyovuja ya simu yalionyesha kuwa Misri iliwasiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel ili kupata baraka na uungaji mkono wake kabla ya kusaini muafaka wa mauziano hayo tata.