Uturuki yaendelea kukiuka mamlaka ya kujitawala Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i86176-uturuki_yaendelea_kukiuka_mamlaka_ya_kujitawala_iraq
Uturuki kwa mara nyingine imekiuka mamlaka ya kujitawala Iraq kwa kuvamia mikoa ya kaskazini mwa nchi hiyo. Jeshi la Uturuki lilifanya shambulio katika kituo cha utalii katika mkoa wa Zakho ulioko katika eneo la Kurdistan ya Iraq Jumatano, na kuwauwa wanawake na watoto wasiopungua 11.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 23, 2022 04:19 UTC
  • Uturuki yaendelea kukiuka mamlaka ya kujitawala Iraq

Uturuki kwa mara nyingine imekiuka mamlaka ya kujitawala Iraq kwa kuvamia mikoa ya kaskazini mwa nchi hiyo. Jeshi la Uturuki lilifanya shambulio katika kituo cha utalii katika mkoa wa Zakho ulioko katika eneo la Kurdistan ya Iraq Jumatano, na kuwauwa wanawake na watoto wasiopungua 11.

Hii sio mara ya kwanza kwa serikali ya Uturuki kuchukua hatua kama hiyo dhidi ya Iraqi katika eneo la Kurdistan.

Kulingana na vituo kadhaa vya habari vya Iraqi, kama vile Saber News, katika kipindi cha miezi 7 iliyopita, serikali ya Uturuki imefanya mashambulio 281 katika mikoa ya Dukuk, Erbil, Sulaimaniyah na Mosul nchini Iraq. Kama kawaida, maafisa wa Uturuki walikariri madai kwamba uwepo wa kundi la Kikurdi la Kituruki (PKK) ndio sababu ya kuyashambulia maeneo ya kaskazini mwa Iraqi.

Kuna nukta kadhaa za uchambuzi kuhusu shambulio la hivi karibuni la Uturuki huko Iraq Kaskazini.

Nukta ya kwanza ni; Shambulio la Uturuki na mauaji ya wanawake na watoto yamepelekea kuwepo kauli moja ya wananchi na maafisa wa Iraq katika kulaani hujuma hiyo ya kijeshi ya Uturuki. Raia wa Iraqi waliokuwa na hasira walishambulia ofisi ya kutoa visa za Uturuki huko Najaf ambapo walishusha bendera ya nchi hiyo.

Waandamanaji huko Baghdad pia walikusanyika mbele ya ubalozi wa Uturuki na, pamoja na kushusha bendera za Uturuki na kuziteketeza moto walipiga nara za kulaani mashambulio ya kijeshi huko kaskazini mwa Iraq na uwepo wa wavamizi katika ardhi ya nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Fuad Hussein

Aidha vituo vya kutoa visa vya Uturuki vilifungwa na watu wenye hasira katika miji ya Iraq ya  Basra na Nasiriyah.

Wakati huo huo, maafisa wa Iraq, wakiwemo Rais, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje, pia wamelaani hatua hiyo ya Uturuki na wakasema watafikisha mashtaka katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Nukta ya pili ni; mbali na madhara ya kibinadamu kufuatia hujuma hiyo ya Uturuki, maafisa wa Iraqi wanaichukulia hatua hiyo kama ukiukaji wa uhuru wake ambao umetekelezwa mara kadhaa na serikali ya Uturuki.

Maafisa wa Iraqi wanaamini kwamba serikali ya Ankara haipaswi kuleta masuala yake ya ndani na changamoto kwenye jiografia ya Iraqi na kwa kisingizio hicho kukiuka mamlaka ya kujitawala Iraq. Kuhusu suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraqi Fuad Hussein ameonya: "Kama kuna tatizo kati ya serikali ya Uturuki na chama cha PKK, tatizo hilo halipaswi kuvutwa ndani ya Iraq." Baraza la Mawaziri la Iraqi pia limesema katika taarifa kwamba linapinga kuanzishwa uvamizi mwingine dhidi ya Iraq, kama ambavyo pia linapinga vikali kundi lolote la kigaidi au wanagambo wenye silaha kutumia ardhi yake kuendesha shughuli zao.

Nukta ya  tatu ni kuwa; Kinyume na yalivyokuwa mashambulio ya zamani ambapo Uturuki haikukana kuhusika nayo, mara hii mauaji ya wanawake na watoto katika shambulio hilo yameipelekea kukana kabisa kutekeleza shambulio kama hilo nchini Iraqi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlüt Çavuşoğlu 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlüt Çavuşoğlu  amesema, "kwa msingi wa habari tuliyopokea kutoka Kikosi cha Anga cha Jeshi, hakukufanyika shambulio lolote dhidi ya raia katika eneo la Dehuk nchini Iraq," 

"Tunapinga tuhuma dhidi yetu na tuko tayari kushirikiana na maafisa wa Iraqi. Kuna makundi kadhaa ya kigaidi, pamoja na Chama cha Wafanyikazi wa Kurdistan (PKK), kwenye ardhi ya Iraq," Çavuşoğlu amesema. Kauli hiyo ya Çavuşoğlu imekuja huku mwenzake wa Iraq Fouad Hussein akisema wataalamu wa jeshi la nchi hiyo wamethibitisha kwamba shambulio hilo lilitokea Uturuki.

Nukta ya mwisho ni kuwa kutokuwepo serikali kuu yenye nguvu Iraq, na vile vile mwendelezo wa mkwamo wa kisiasa kati ya makundi ya Iraq, ni jambo muhimu ambalo yamkini limeifanya Uturuki kuwa na ubavu wa kukariri mashambulio dhidi ya nchi hiyo jirani.