Hamas: Mapambano dhidi ya maghasibu yataendelea hadi Palestina itakapokombolewa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i88084-hamas_mapambano_dhidi_ya_maghasibu_yataendelea_hadi_palestina_itakapokombolewa
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetoa taarifa kwa nasaba wa kutimia mwaka wa 17 wa kutimuliwa Wazayuni kutoka Ukanda wa Gaza, ikisisitiza kuendelezwa mapambano ya Wapalestina hadi malengo yao ya mwisho yatakapofikiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 12, 2022 10:44 UTC
  • Hamas: Mapambano dhidi ya maghasibu yataendelea hadi Palestina itakapokombolewa

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetoa taarifa kwa nasaba wa kutimia mwaka wa 17 wa kutimuliwa Wazayuni kutoka Ukanda wa Gaza, ikisisitiza kuendelezwa mapambano ya Wapalestina hadi malengo yao ya mwisho yatakapofikiwa.

Miaka 17 iliyopita yaani tarehe 15 Agosti 2005, Wazayuni walilazimika kuondoka katika vitongoji 21 vya walowezi eneo la Gaza kufuatia mapambano ya wanamuqawama wa Kipalestina.

Vitongoji hivyo vilikuwa na jumla ya wakazi elfu 8 na vilijengwa kwenye ardhi iliyoghusubiwa ya Palestina yenye ukubwa wa kilomita za mraba 36 za eneo la Ukanda wa Gaza. Gaza ina eneo la kilomita za mraba 360, na vitongoji hivyo  vilichukua moja ya kumi ya eneo la Gaza.

Taarifa iliyotolewa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina imesema: "Mchakato wa harakati ya muqawama wa kishujaa huko Palestina unaendelea katika njia iliyonyooka, madhubuti na kwa imani thabiti juu ya uhalali wa mapambano hayo na uadilifu wa kadhia ya Palestina."

Hamas imeongeza kuwa: "Miaka 15 imepita tangu kuanza mzingiro wa pande zote dhidi ya watu wa Gaza; mzingiro huu ni uhalifu dhidi ya binadamu na doa chafu kwenye vipaji vya nyuso za watu wanaonyamaza kimya na wasiosimama kupinga, kulaani na kujaribu kukomesha uhalifu huu."

Taarifa ya Hamas imeongeza kuwa, taifa la Palestina halitanyamaza kimya mbele ya matokeo na athari mbaya za mzingiro hatari wa Gaza.

Mwishoni mwa taarifa hiyo, harakati ya Hamas sambamba na kulaani mipango ya utawala wa Kizayuni ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi na Kuyayahudisha maeneo ya Kipalestina na Kiislamu, imesisitiza ulazima wa kuundwa nchi huru ya Palestina, ambayo mji mkuu wake ni Quds tukufu. Vilevile imezitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu kufanya juhudi kubwa za kukomesha mzingiro wa Gaza.

Ikumbukwe kuwa, kuondoka kwa madhila kwa Wazayuni katika eneo la Ukanda wa Gaza ilikuwa hatua iliyoleta mabadiliko makubwa katika harakati ya kupigania uhuru wa Palestina na katika kupanuka kwa mapambano dhidi ya utawala huo ghasibu.