Baraza jipya la mawaziri la Netanyahu na changamoto zilizopo
Benjamin Netanyahu alitangaza katika dakika za mwisho za muda wake wa mwisho kisheria wa kutangaza serikali kwamba alikuwa amefanikiwa kuunda baraza jipya la mawaziri la utawala haramu wa Israel.
Netanyahu alitangaza Jumatano usiku kupitia ujumbe wa Twitter ikiwa ni dakika chache kabla ya kumalizika makataa rasmi aliyopewa kubuni serikali, kwamba alikuwa amefikia makubaliano na vyama vya muungano kuunda baraza la mawaziri.
Akiwa amehudumu katika nafasi ya waziri mkuu wa Israel kwa miaka 15, Benjamin Netanyahu anashikilia rekodi ya kukaa kwa muda mrefu zaidi katika nafasi hiyo katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina. Hii ni mara ya tatu ambapo anakuwa waziri mkuu wa baraza la mawaziri la utawala huo wa kibaguzi. Netanyahu alihudumu kwa mara ya kwanza katika nafasi hiyo mwaka 1996 kwa kipindi cha miaka 3, mara ya pili kuanzia 2009 hadi 2021 kwa muda wa miaka 12 na sasa anahudumia nafasi hiyo kwa mara ya tatu.
Hata hivyo, uwaziri mkuu wa Netanyahu katika kipindi hiki ni tofauti na mihula miwili ya kwanza na kwa ujumla miaka 15 iliyopita kwa sababu katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 1996 hadi 1999 na mwanzoni mwa muhula wa pili kuanzia 2009, utawala wa Israel haukushuhudia hali ya mkwamo wa kisiasa kama ilivyo sasa. Netanyahu na baraza lake jipya la mawaziri wameibuka kutoka kwenye mkwamo wa kisiasa uliodhihiri miaka 4 iliyopita katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Katika miaka 4 iliyopita, chaguzi 5 za bunge zimefanyika katika ardhi hizo ambapo umri wa serikali haukutimia hata mwaka mmoja.
Kwa hivyo, hali hiyo bado ni changamoto muhimu ya kisiasa kwa baraza jipya la mawaziri la Israel kwa sababu wapinzani wake wakuu hawataacha juhudi za kujaribu kuingia madarakani na kuvuruga shughuli za baraza jipya la mawaziri litakalobuniwa na Netanyahu, jambo ambalo Netanyahu mwenyewe pia alilifanya dhidi ya baraza la mawaziri la muungano wa Naftali Bennett na Yair Lapid. Kuhusiana na suala hilo, Yair Lapid aliwaambia mawaziri wake katika mkutano wake wa mwisho na baraza la mawaziri kwamba; 'tutarejea kwenye chumba hiki hivi karibuni.'
Tofauti nyingine kati ya muhula mpya wa Netanyahu kama waziri mkuu na mihula miwili ya awali ni muungano wake na watu wenye itikadi kali za mrengo wa kulia. Chama cha kihafidhina cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu, pamoja na vyama vya kidini vya Orthodox na walowezi wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, walishinda viti 64 kati ya viti 120 vya bunge la Israel katika uchaguzi wa hivi karibuni. Kuunda baraza la mawaziri na watu wenye misimamo mikali ni mojawapo ya changamoto kubwa zinazomkabili Netanyahu katika utawala wake mpya.
Netanyahu mwenyewe ni mmoja wa watu wanaoibua mivutano zaidi katika utawala haramu wa Israel, na katika kipindi hiki kipya, Wazayuni wenye msimamo mikali pia wameungana naye ili kubuni serikali mpya. Kuwepo kwenye serikali hiyo watu wenye misimamo mikali kama vile Itamar Ben Gvir kutoka chama chenye nguvu cha Mayahudi, ambaye kwa mujibu wa ripoti za kuaminika atakuwa Waziri wa Usalama wa Ndani na hivyo kudhibiti polisi, kumefanya baadhi ya watu waamini kwamba baraza jipya la mawaziri la Netanyahu halitadumu kwa muda mrefu. Kwa hakika, katika baraza hilo jipya la mawaziri, waungaji mkono wa siasa za mrengo wa wastani hawana nafasi yoyote muhimu.
Tofauti nyingine kati ya uwaziri mkuu mpya wa Netanyahu na mihula miwili iliyopita inahusiana na mazingira ya nje. Katika duru mbili za kwanza, makundi ya mapambano ya Kiislamu hayakuwa na nguvu kama ilivyo sasa. Leo makundi ya muqawama yako kwenye kilele cha nguvu na katika miezi michache iliyopita, makundi 7 mapya ya mapambano yameundwa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu ambayo yana nia na azma kubwa ya kukabiliana vilivyo na jinai za utawala wa Kizayuni.
Kwa hivyo, iwapo utawala huo utaendelea na jinai zake dhidi ya Wapalestina na watu wenye mimano mikali katika utawala wa Kizayuni kuendeleza siasa zao za ukatili dhidi ya Wapalestina, ni wazi kuwa harakati za mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni zitaongezeka, na bila shaka hiyo itakuwa changamoto kubwa ya kiusalama kwa baraza jipya la mawaziri la Netanyahu.