Hizbullah: Ndoto ya Netanyahu ya kuanzisha muungano dhidi ya Iran haikuaguka
Naibu Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema: matukio ya hivi karibuni ya Palestina na eneo na milingano uliolazimishwa kuwepo na Muqawama vimezima ndoto ya Netanyahu ya kuanzisha muungano dhidi ya Iran.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Al-Ahad, Sheikh Ali Daamush, Naibu Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon ameeleza kwamba: matukio ya eneo, hususan kukaribiana Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kurejea Waarabu nchini Syria, vimeteteresha mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na kuvuruga ndoto ambayo Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni alikuwa akiiwaza kwa muda mrefu ya kuunda muungano wa kieneo na baadhi ya nchi za Kiarabu zikiongozwa na Israel, dhidi ya mhimili wa Muqawama na Iran.
Daamush ameeleza kuwa mhimili wa muqawama uliweza kuziwekea mzingiro medani za Wazayuni kwa kutumia ndege zisizo na rubani na kambi za umoja, na akaongeza kuwa, matukio ya hivi karibuni ya Palestina yamedhibiti ukorofi wa adui Mzayuni wa kuendeleza uchokozi na kuonyesha utete na udhaifu wa utawala wa Kizayuni katika kukabiliana na muqawama; na mkabala wake, yameonyesha kuwa muqawama uko imara, umejipanga na unafanya kazi kwa uratibu wa pande zake zote.
Afisa huyo wa Hizbullah amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni umenasa kwenye mzingiro na milingano wa nguvu uliowekwa na muqawama na uko kwenye mkondo wa kudhoofika, wakati mhimili wa muqawama unaendelea kuwa na nguvu zaidi.
Hivi sasa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umepatwa na kiwewe na hofu kubwa kutokana na kutibuka hali ya mambo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na unafanya kila uwezalo ili kudhibiti hali ya eneo hilo.../