Asilimia 97 ya maji katika nyumba za Ukanda wa Ghaza, hayanyweki
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i98508-asilimia_97_ya_maji_katika_nyumba_za_ukanda_wa_ghaza_hayanyweki
Mkurugenzi wa Taasisi ya Maji ya Ghaza ameeleza kuwa: Asilimia 97 ya maji katika nyumba za raia wa Palestina wa Ukanda wa Ghaza hayanyweki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 07, 2023 07:16 UTC
  • Asilimia 97 ya maji katika nyumba za Ukanda wa Ghaza, hayanyweki

Mkurugenzi wa Taasisi ya Maji ya Ghaza ameeleza kuwa: Asilimia 97 ya maji katika nyumba za raia wa Palestina wa Ukanda wa Ghaza hayanyweki.

Shirika la habari la Mehr la nchini Iran limevinukuu vyombo vya habari vya Palestina na kuripoti kuwa, Munzir Salim Mkurugenzi wa Taasisi ya Maji ya Ukanda wa Ghaza amesema kuwa asilimia 97 ya maji katika nyumba za Wapalestina wakazi wa Ukanda wa Ghaza hayanyweki na kutahadharisha juu ya madhara yanayoweza kusababishwa na maji hayo kwa Wapalestina zaidi ya miloni mbili wa eneo hilo.  

Munzir Salim ameongeza kuwa, maji ya mabomba ya nyumba za Wapalestina katika Ukanda wa Gaza hayanyweki, na wanayatumia kwa shughuli nyingine za nyumbani. 

Amesema, hali hii tajwa ni kengele ya hatari inayoashiria ukosefu wa vyanzo vya maji salama kwa ajili ya raia wa Palestina wa Ukanda wa Ghaza ikiwa ni pamoja na maji ya chini ya ardhi na vyanzo vingine mbadala.  

Huduma ya maji kwa raia wa Palestina wa Ukanda  wa Ghaza si salama 

Mzingiro wa zaidi ya miaka 16 wa utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza  umekuwa na taathira hasi na kuzidisha matatizo kwa maisha ya raia wa Palestina zaidi ya milioni mbili wa eneo hilo.