Wanamuqawama wa Palestina watekeleza oparesheni 22 dhidi ya Wazayuni
Wanamapambano wa Palestina jana walitekeleza oparesheni 23 dhidi ya Wazayuni ikiwa ni katika kuendeleza hatua za wanamuqawama wa Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Shirika la habari la Shihab la Palestina limeripoti kuwa, Kituo cha Takwimu na Habari cha Palestina kimetangaza kuwa wanamapambano wa Palestina jana siku nzima waliwashambulia wanajeshi wa utawala Kizayuni wa Israel katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds inayokaliwa kwa mabavu kwa kuwafyatulia risasi na kurusha vifurushi vya miripuko.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, wanamuqawama wa Palestina walitekeleza oparesheni huko Quds, Nablus, Ramallah, Jenin, Bait -Laham, Tulkarm na al Khalil, na kukabiliana na mashambulizi ya Wazayuni. Awali, televisheni ya 7 ya utawala wa Kizayuni wa Israel ilikuwa imetangaza kuwa, mwezi uliopita oparesheni 124 za ufyatuaji risasi zilitekelezwa katika Ukingo wa Magharibi na Quds inayokaliwa kwa mabavu.
Mwezi Aprili pia Wazayuni watatu waliangamizwa na wengine 41 kujeruhiwa katika mapigano katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Wapalestina 11 pia waliuliwa shahidi katika mapigano hayo.
Hali ya mambo hivi sasa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina hasa katika Ukingo wa Magharibi ni makhsusi mno, kwa sababu wanamapambano wa Palestina wamekuwa wakijibu jinai zisizohesabika za Wazayuni kwa kutumia kila wenzo; jambo limeibua hali ngumu kwa Wazayuni.